Lochakapong ataka swala la uchimbaji madini kutoingiza siasa Pokot magharibi

Na Benson Aswani,
Mjumbe wa sigor kaunti ya Pokot magharibi Peter lochakapong amewasuta baadhi ya viongozi wa kisiasa katika kaunti hiyo kwa kile amedai wameingiza siasa katika swala zima la uchimbaji madini maeneo ya lami nyeusi na kambi karai.
Akizungumza katika eneo bunge lake, Lochakapong alimkashifu kiongozi mmoja kaunti hiyo akidai anawachochea wananchi dhidi ya viongozi hasa baada ya kumhusisha yeye na shughuli za mwekezaji mmoja wa uchimbaji madini.
“Kuna wanasiasa katika kaunti hii ambao wameingiza siasa kwenye swala la uchimbaji madini eneo la Kambi Karai na lami nyeusi. Hao viongozi wamewadanganya wakazi sehemu hizo na kuwachgochea dhidi ya viongozi wao. Nataka kuwaambia kwamba watafute mbinu nyingine ya kuendeleza siasa,” alisema Lochakapong.
Pia lochakapong alisema kabla ya uchimbaji madini kuendelea katika kaunti hiyo kulikuwa na ushiriki wa umma ambao ulifanywa na wananchi pamoja na mwekezaji huyo, na wananchi wakamkubali kuendeleza shughuli zake za uchimbaji madini.
“Mimi mwenyewe niliongea na watu wangu wa Nasolot, Lami nyeusi na kambi Karai, wakaniambia kwamba kuna mtu amefika, ameongea na sisi na tumekubaliana na yeye kutufanyia mambo kadhaa hapa. Na mimi kama kiongozi wao basi nikasema huyu ndiye watu wangu wamekubali,” alisema.
Kauli yake Lochakapong ilijiri siku chache tu baada ya mbunge wa Pokot kusini David Pkosing kumhusisha na mwekezaji anayeendeleza shughuli ya uchimbaji madini maeneo hayo Okech Salah, ambaye alimshutumu kwa kile alidai amewafurusha wakazi maeneo ambako wamekuwa wakiendeleza shughuli hiyo ya uchimbaji madini.
