Kubuniwa hazina ya miundo mbinu ni hatua muhimu kwa safari ya Kenya kufikia Singapore; Poghisio

Na Benson Aswani,
Hatua ya baraza la mawaziri kubuni hazina ya miundo mbinu (infrastructure fund) inadhihirisha umakini wa serikali chini ya uongozi wa rais William Ruto kuhakikisha kwamba uchumi wa taifa hili unaimarika na kufikia viwango vya mataifa yaliyoendelea (first world countries).
Haya ni kwa mujibu wa aliyekuwa seneta wa kaunti ya Pokot magharibi Samwel Poghisio ambaye alisema licha ya azma hiyo ya rais William Ruto kuonekana kuwa ndoto machoni pa wengi, hatua hiyo ya baraza la mawaziri ni ishara muhimu kuelekea maazimio hayo.
“Haya mambo ambayo yalipitishwa na mawaziri ni muhimu sana katika nchi hii ya Kenya. Na hiyo sisi wengine tukiangalia pengine tunaona ugumu wake. Lakini nafikiri baraza la mawaziri wameamua na kwa hivyo imepitishwa ya kwamba hili litafanyika,” alisema Poghisio.
Poghisio alisema ni jukumu sasa la serikali kubainisha jinsi ambavyo kiasi cha shilingi trilioni 5 ambacho kinakadiriwa kuwazesha juhudi hizi kitapatikana, ikizingatiwa ni kiasi kikubwa zaidi kuwahi kupangiliwa miradi ya maendeleo nchini.
“Naamini ya kwamba baraza la mawaziri na rais wataendelea kutuonyesha njia ambayo tutafanya ili tupate fedha hizi. Unajua bajeti yetu ya mwaka mmoja hapa Kenya sasa hivi ni trilioni 3 kufanya kila kitu. Na hivyo trilioni 5 itakuwa hazina ya kipkee katika Kenya hii,” alisema.
Hata hivyo Poghisio alielezea wasiwasi wa hulka ya viongozi wa taifa hili kutokuwa na nidhamu katika kutekeleza maswala ya maendeleo licha ya kuwepo raslimali hitajika, kuwa huenda kikawa kikwazo cha kuafikia azimio hilo la kufanya Kenya kufikia mataifa ya daraja la kwanza.
