Kampuni ya kutengeneza mfumo wa upitishaji maji taka yalaumiwa kwa kutelekeza miradi ya maendeleo Kaplelach Koror

Na Emmanuel Oyasi,
Wakazi eneo la Kaplelach koror eneo bunge la Kapenguria kaunti ya Pokot magharibi wamelalamikia kutelekezwa miradi ambayo inapaswa kutekelezwa na kampuni ambayo imepewa kandarasi ya kutengeneza mfumo wa upitishaji maji taka wa Kapenguria -Makutano.


Wakiongozwa na Reuben Loitang’or, wakazi hao walisema licha ya kuwasilisha miradi ambayo wanataka itekelezwe na kampuni hiyo inavyohitajika kisheria, hamna hatua ambayo imechukuliwa na kampuni hiyo kufikia sasa.

“Tulikubaliana na kampuni hii kwamba tunahitaji madarasa manne na maji. Lakini tangu tulipokubaliana kuhusu miradi hii, hamna chochote ambacho kimefanyika kufikia sasa, na wako wanamaliza kazi yao huku” alisema Loitang’or


Kauli yao ilisisitizwa na viongozi wa kisiasa kutoka eneo hilo wakiongozwa na mbunge wa Kapenguria Samwel Moroto ambao kando na kulalamikia kutotekelezwa mradi wowote na kampuni hiyo, walikosoa kiwango cha fedha ambacho kimetengewa miradi ikilinganishwa na fedha ambazo kampuni hiyo ilitengewa kwa kandarasi iliyokabidhiwa.


“Kama viongozi katika kaunti hii hatujafurahia jinsi kampuni hii imeshughulikia maendeleo kwa ajili ya jamii ya hapa. Kwa sababu kulingana na makubaliano yao na jamii, tumepokea malalamishi kwamba walihadaiwa na kampuni hii,” alisema Moroto.


Kwa upande wake mwenyekiti wa shirika la maji, kazi na maendeleo kaskazini mwa bonde la ufa Prof. John Lonyangapuo aliahidi kushirikiana na wadau mbali mbali kufuatilia swala hilo ikiwemo kuandaa kikao na viongozi wa kampuni hiyo kuhakikisha kwamba wakazi wa maeneo hayo wanahudumiwa inavyopasa.


“Mimi kama mwenyekiti nimeahidi kwamba nitafuatilia, nikutane na mwenyekiti mwenzangu wa Nakuru pamoja na viongozi kutoka hapa, tuketi na uongozi wa kampuni hii watuelezee ukweli kuhusu swala hili,” alisema Lonyangapuo.