KAMPENI YA KUHAKIKISHA WATOTO WOTE WANAENDA SHULE YAENDELEA POKOT MAGHARIBI.
Wito umetolewa kwa wazazi katika kaunti ya Pokot magharibi kuhakikisha kwamba wanao waliofanya mtihani wa KPSEA na wa darasa la nane KCPE wanajiunga na viwango ambavyo wanapasa kuendeleza masomo yao.
Mkurugenzi wa elimu kaunti hiyo Simon Wamae alisema kwamba masomo ya shule za sekondari ya msingi yamethaminiwa na serikali na hamna sababu ya mzazi kusalia nyumbani na mwanawe kwa kisingizio cha kukosa karo au sare ya shule.
“Tunawasihi wazazi ambao wana watoto katika shule za sekondari ya msingi kuwapeleka wanao shuleni kwani serikali imegharamia masomo yao. Swala la Sare pia lisiwe sababu ya watoto kusalia nyumbani kwani serikali imeagiza kila mwanafunzi aingie shuleni akiwa na sare aliyokuwa nayo wakati mzazi anaendelea kujipanga kutafuta sare ya shule hiyo.” Alisema Wamae.
Aidha wamae alitaka wanafunzi ambao walifaa kujiunga na kidato cha kwanza ila wakakosa fursa hiyo kutokana na tatizo la karo kusajiliwa katika shule za kutwa, ili kuhakikisha kwamba agizo la serikali la wanafunzi wote kuhudhuria masomo linafanikishwa.
“Wazazi wa wanafunzi waliopasa kujiunga na kidato cha kwanza na wangali nyumbani kwa ajili ya karo, wawasajili wanafunzi hao katika shule za kutwa na waendelee na masomo kwani serikali imesema elimu katika shule hizo ni bure.” Alisema.
Hata hivyo Wamae alisema asilimia 94 ya wanafunzi wamejiunga na kidato cha kwanza huku wale ambao wamejiunga na shule za sekondari ya msingi wakiwa asilimia 98, juhudi zikiendelezwa kuhakikisha wanafunzi wote wanaenda shule.
“Kufikia sasa ni asilimia 94 ya wanafunzi ambao wamejiunga na kidato cha kwanza huku asilimia 98 wakijiunga na shule za sekondari ya msingi. Tunashirikiana na wadau wote kuhakikisha wanafunzi wote wameenda shuleni.” Alisema.
Na Benson Aswani.