Kachapin awasuta wanaokosoa utendakazi wake

Na Benson Aswani,
Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin ametetea utendakazi wa serikali yake kutokana na shutuma ambazo zinaibuliwa na baadhi ya viongozi kaunti hiyo kwamba hamna lolote ambalo ametekeleza katika awamu yake ya pili ya uongozi.


Akizungumza na wanahabari, gavana Kachapin aliwasuta viongozi ambao wanaeneza madai kwamba hajatekeleza miradi yoyote ya mendeleo kwa ajili ya wakazi akiwataja kuwa viongozi wanaoendeleza siasa potovu ili kujipatia umaarufu wa kisiasa.

Gavana Kachapin aliwataka wakazi wa kaunti hiyo kuwapuuza viongozi kama hao na kuwa makini sana wakati wa uchaguzi ili kuwachagua viongozi wenye nia ya kuwahudumia wananchi, wala si kueneza propaganda za kuwaharibia sifa viongozi wenzao machoni pa wananchi.


“Kuna baadhi ya viongozi katika kaunti hii ambao wamezoea kupata viti kwa kusema uongo na kueneza propaganda. Kusema kwamba sijafanya lolote ni kuwahadaa wananchi. Ukitembea hapa utaona maendeleo mengi ambayo nimeweza kutekeleza,” alisema Kachapin.

Gavana Kachapin alisema yapo mengi ambayo yameafikiwa katika kaunti hiyo chini ya uongozi wake hasa sekta ya afya ambayo alisema sasa kuna dawa za kutosha katika vituo vya afya, pamoja na wahudumu wa afya wa kutosha.


Alimtaka seneta wa kaunti hiyo kuwalezea wananchi kile ambacho amefanya kuhakikisha kwamba serikali ya kaunti inapata mgao wa kutosha.


“Juzi tumepeana madawa, tumeandika wahudumu wa afya wa kutosha, na kwa kuwa seneta wa kaunti hii anasema kwamba sijafanya lolote, nataka yeye atueleze tangu achukue hatamu miaka mitatu iliyopita, West Pokot tumepata mgao kiasi gani? Kwa sababu sisi tungali chini sana kwa mgao,” alisema Kachapin.