Kachapin awaonya vikali wachimba madini Pokot magharibi

Na Emmanuel Oyasi,
Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin ametoa onyo kwa wawekezaji ambao wanaendeleza uchimbaji wa madini katika kaunti hiyo bila ya kufuata taratibu ambazo zinafaa.
Gavana Kachapin alisema raslimali za kaunti hiyo zimeharibiwa pakubwa na wawekezaji aliodai wanatumia mbinu zisizokubalika kuchimba madini, hali ambayo imepelekea kuharibiwa mazingira ya maeneo ambako shughuili hiyo inatekelezwa.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya madaraka, katika uwanja wa shule ya msingi ya Makutano eneo bunge la Kapenguria, gavana Kachapin alitoa wito kwa idara ya usalama kaunti hiyo kushirikiana na serikali katika kuhakikisha shughuli ya uchimbaji haramu wa madini inasitishwa.
“Bado tunatoa ilani kwa wale wanaokuja kuharibu mazingira yetu na raslimali zetu kupitia uchimbaji madini. Iwapo serikali haitachukua hatua, basi itatulazimu sisi wenyewe tuchukue hatua ya kuwafukuza,” alisema gavana Kachapin.
Gavana Kachapin alisema raslimali nyuingi ambazo zingetumika kuimarisha hali ya kaunti ya Pokot magharibi zinapotea mikononi mwa wawekezaji wachache ambao hawana nia njema na wakazi wa kaunti hiyo, hali aliyosema kamwe haitakubalika.
“Tunapasa kupigania raslimali hizi ili zijenge barabara zetu, zijenge shule zetu na kuimarisha kaunti hii. Si mtu kuja na kuchukua sehemu yote, akichukua wazee wachache na kuwapeleka hotelini ili aendelee kuharibu raslimali zetu,” alisema.
Gavana Kachapin vile vile aliwasuta baadhi ya viongozi aliodai wanashirikiana na wawekezaji hao kuharibu raslimali alizosema zingetumika kuimarisha hali ya kaunti hiyo ya Pokot magharibi.
“Na mimi nimeambiwa pia kwamba hata kuna wabunge ambao wanashirikiana na wawekezaji hawa,” aliongeza.
