Kachapin awaonya maafisa ‘wazembe’ katika serikali yake

Na Benson Aswani,
Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin ameendelea kusisitiza kwamba kamwe hataruhusu maafisa wazembe katika serikali yake.


Akizungumza katika katika kikao na wanahabari, Gavana Kachapin alisema atatumia kipindi cha miezi mitatu kuanzia Januari mwakani kutathmini utendakazi wa maafisa wapya ambao waliapishwa majuzi, akionya kwamba watakaokosa kutekeleza kazi zao ifaavyo watafukuzwa kazi.

Gavana Kachapin alisema serikali yake inatumia fedha nyingi kugharamia mishahara ya wafanyikazi wa umma na kamwe hataruhusu maafisa ambao watafurahia tu mishahara bila ya kuleta matokeo katika idara wanazohudumu.


“Nitaendelea kusema kwamba, watu wazembe katika serikali yangu sitawapatia nafasi ya kuhudumu. Nilijibwaga uwanjani kutafuta ugavana na nikatafuta wasaidizi ambao watanisaidia kufanya kazi. Lakini wale wazembe nitakabiliana nao, na nimeanza tayari,” alisema gavana Kachapin.


Wakati uo huo gavana Kachapin alisema serikali yake imetekeleza miradi mingi katika kipindi ambacho amekuwa mamlakani, ambayo ataizindua mwaka ujao ili ianze kuwafaidi wananchi kabla ya kuanza siasa za uchaguzi mkuu ujao.


“Kuna miradi mingi ambayo tumetekeleza katika miaka mitatu iliyopita katika idara ya maji, idara ya afya, barabara, elimu na kadhalika. Kwa hivyo nimesema mwaka ujao nitaweka muda wangu mwingi kutembea na kufungua hiyo miradi, kwa sababu tukichelewa hatutamaliza,” aliongeza.