Kachapin atoa hakikisho la huduma za afya kuimarika Pokot magharibi

Na Benson Aswani,
Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin ameendelea kupongeza hatua ya kusitishwa mgomo wa wauguzi katika kaunti hiyo baada ya chama cha maafisa hao kuandaa mazungumzo na serikali ya kaunti.
Akizungumza baada ya kupokea dawa za kima cha shilingi milioni 81 kutoka kwa shirika la kusambaza dawa la KEMSA, gavana Kachapin aliendelea kusisitiza kwamba serikali yake itahakikisha kuwa maswala waliyokubaliana na wauguzi hao yatatekelezwa kikamilifu.
Aidha gavana Kachapin alisema dawa hizo zimewadia wakati mzuri ambapo huduma za afya zimerejelewa kikamilifu katika hospitali za umma, na kwamba zitasaidia pakubwa katika kuimarisha huduma kwa wananchi.
“Wauguzi na maafisa wa kliniki walikuwa kwenye mgomo kwa karibu wiki tatu, lakini kupitia mazungumzo walitusikiliza na kurejea kazini. Kwa hivyo mimi nawataka tu wafanye kazi vizuri kwa kuwa yale tuliyokubaliana lazima tutayatimiza,” alisema gavana Kachapin.
Gavana Kachapin aliwahimiza wahudumu hao wa afya kujitolea kikamilifu katika kutoa huduma kwa wakazi, serikali inapoendelea kujitahidi kutimiza matakwa yao na kuhakikisha kwamba sekta ya afya inaimarika hata zaidi.
“Wito wangu ni kwamba tuwasaidie watu wetu. Jambo la muhimu ni huduma kwa raia. Hamna jambo muhimu katika dunia kama kutumikia watu. Kuna furaha kubwa katika kuhakikisha mwananchi anapata huduma iliyo bora,” alisema.
