Kachapin atakiwa kuangazia lalama za wanafunzi kuhusu basari

Na Emmanuel Oyasi,
Mbunge wa Kapenguria Samwel Moroto ametoa wito kwa gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin kuangazia lalama ambazo zinatolewa na baadhi ya wanafunzi wa shule za upili na vyuo vikuu kuhusiana na mgao wa fedha za basari ambazo zilizinduliwa hivi majuzi na serikali yake.
Akizungumza na kituo hiki, Moroto alisema litakuwa jambo la busara kwa gavana kachapin kufanya kikao na wanafunzi hao ili kusikiliza lalama zao na kisha kuangazia jinsi ambavyo ataweza kuzishughulikia na kuzuia hali kwamba baadhi yao huenda wakakosa kufuzu kufuatia changamoto ya karo.
Aidha Moroto alisema swala la elimu ni moja ya ajenda kuu ambazo alizipigia debe gavana Kachapin wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita, na anapasa kutumia fursa hii kuhakikisha kwamba elimu inaimarika chini ya utawala wake.
“Nimesikia tangu juzi wanafunzi wa shule za upili na vyuo vikuu wanalalamika kuhusu jinsi fedha za basari zinatolewa. Kwa hivyo namwomba gavana wetu kushuka chini na kuzungumza na wanafunzi hawa ajue mahali shida iko ili arekebishe mara moja,” alisema Moroto.
Moroto alielezea umuhimu wa fedha hizo za basari akisema kwamba wapo wengi wa wanafunzi ambao wanatoka katika jamii zisizojiweza kifedha, na tegemeo lao la pekee kuafikia ndoto zao maishani ni kupitia ufadhili wa basari.
“Wapo wanafunzi wengi kutoka jamii masikini ambao wanategemea fedha za basari, na iwapo hawatapata fedha hizo wataathirika sana katika masomo yao,” alisema.