Kachapin apongeza juhudi za viongozi waliopigania ugatuzi

Na Benson Aswani,
Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin amepongeza mashujaa anaosema walipigania ukombozi wa pili wa taifa, hali iliyopelekea kuwepo serikali za magatuzi ambazo zimeleta manufaa makubwa kwa wananchi hasa maeneo ya mashinani.
Akizungumza katika hafla ya maadhimisho ya siku ya mashujaa ambayo iliandaliwa katika uwanja wa shule ya msingi ya Makutano, gavana Kachapin alisema ni kupitia ugatuzi ambapo sekta muhimu kama vile afya miongoni mwa zingine zimeweza kuimarika.
“Katika kaunti yetu, unaona zahanati zimetapakaa kila mahali, kuna dawa na wauguzi wa kutosha. Haya ni matokeo ya ugatuzi ambao ulipiganiwa na viongozi wetu waliopigania ukombozi wa pili,” alisema Kachapin.
Aidha Kachapin aliwataka viongozi kuiga mfano wa aliyekuwa waziri mkuu hayati Raila Odinga ambaye kulingana naye alikuwa mwepesi wa kufanya kazi na watu waliofikirika kuwa mahasimu wake, na kujitenga na malumbano ya kisiasa kwa manufaa ya maendeleo ya kaunti hiyo.
“Tumesema leo tunaiga mambo ya Raila Odinga ambaye alikuwa mtu aliyefanya kazi hata na wale ambao alikuwa akishindana nao. Tuwache mashindano ya mwaka 2027 na tuhakikishe kwamba tunawahudumia wananchi,” alisema.
Kwa upande wake kamishina wa kaunti hiyo Khalif Abdulahi alipongeza hali ya usalama ambayo imeendelea kushuhudiwa mipakani pa kaunti hiyo ambako kumekuwa na changamoto hiyo kwa muda, akidokeza mipango ya kutumwa maafisa zaidi wa NPR maeneo hayo ili kudumisha hali hiyo.
“Tumekuwa na usalama katika mipaka yetu ya Turkana, Elgeyo Marakwet, Baringo na hata taifa jirani la Uganda. Na ili kudumisha hali hii, tunalenga kuwatuma maafisa zaidi wa NPR ili kusaidia katika doria maeneo hayo,” alisema Khalif.
