Jamii ya Sengwer yataka kuzingatiwa katika nyadhifa za ajira

Wazee wa Jamii ya Sengwer katika kaunti ya Pokot magharibi,Picha/Maktaba

Na Benson Aswani,
Jamii ya Sengwer katika kaunti ya Pokot magharibi imeitaka serikali kuitengea nyadhifa za kazi wakati wa zoezi la kuwaajiri vijana katika idara ya magereza linalotarajiwa hivi karibuni.


Ikiongozwa na msemaji wake Dickson Rotich, Jamii hiyo imesema, kwa muda imekuwa ikitengwa kila wakati kunapoendeshwa zoezi la kutoa ajira kutokana na uchache wake katika kaunti ambako inapatikana swala ambalo ni kinyume cha katiba.


“Tumesikia kwamba idara ya magereza itawaajiri vijana hivi karibuni. Natoa wito kwa serikali kuona kwamba wakati wanapoajiri vijana, jamii ya Sengwer inatengewa nafasi kama jamii ya wachache ama iliyotengwa,” alisema Bw. Rotich.


Alisema hulka ya nafasi za ajira kutolewa kwa misingi ya kufahamiana imeathiri pakubwa jamii hiyo, akiitaka serikali kuzingatia katiba katika shughuli ya utoaji ajira.


“Kwa muda mrefu kumekuwa na hulka mbaya hapa nchini ambapo ajira zinatolewa kwa kufahamiana. Hii tabia inafaa kukoma na serikali izingatie katiba katika swala la kutoa ajira,” alisema.


Wakati uo huo Rotich aliitaka serikali kuharakisha mpango wa kubuniwa divisheni ambayo itatumika kuhudumia jamii hiyo ya Sengwer eneo la Siyoi pamoja na kaunti zingine ambazo jamii hiyo inapatikana.


“Kuna divisheni ambayo inafaa kufunguliwa eneo la Siyoi. Natoa wito kwa serikali kuharakisha kubuni divisheni hiyo ili iweze kushughulikia jamii ya Sengwer katika kaunti zote ambazo jamii hii inapatikana,” aliongeza.