Idara ya usalama Pokot magharibi yakemea mauaji ya raia eneo la Ramos

Na Benson Aswani,
Idara ya usalama katika kaunti ya Pokot magharibi inaendeleza mikakati ya kuhakikisha kwamba visa vya uvamizi ambavyo vimechipuka upya hasa katika mpaka wa kaunti hiyo na kaunti jirani ya Turkana vinakabiliwa.


Kamishina wa kaunti hiyo David Saruni alisema tayari wameandaa kikao na wakuu wa usalama kutoka pande zote mbili na kukubaliana kuhusu maswala kadhaa ikiwemo kuongeza idadi ya maafisa wa usalama maeneo hayo.

Aidha Saruni alisema wameandaa kikao na baraza la wazee ambapo wamekubaliana kuandaa mkutano wa usalama wa jamii kutoka pande zote mbili kama moja ya mikakati ya kuhakikisha swala la utovu wa usalama linashughulikiwa.


“Tumeandaa kikao na wadau wa usalama wa pande zote mbili na kuelewana kwamba tuongeze idadi ya maafisa wa usalama maeneo ya mipakani. Tunapanga pia kuwa na kikao cha wakazi wa jamii zote mbili ili tuangazie hasa kiini cha kuchipuka tena uvamizi huu,” alisema Saruni.


Wakati uo huo Saruni alisema oparesheni ya kutwaa silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria na baadhi ya wakazi bado inaendelea katika kaunti zote za bonde la kerio, katika juhudi za kuhakikisha hamna mkazi anayemiliki bunduki bila kibali rasmi.


“Zoezi la kutwaa silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria na baadhi ya wakazi linaendelea katika kaunti zote za bonde la Kerio, lengo likiwa kuhakikisha hamna bunduki inasalia mikononi mwa raia bila kibali rasmi,” alisema.


Yanajiri haya huku tume ya uwiano na utangamano wa kitaifa (NCIC) ikielezea kusikitishwa na kuchipuka tena visa vya uvamizi na mauaji kwenye mipaka ya kaunti hizo mbili.


Mshirikishi wa tume hiyo eneo la kaskazini mwa bonde la ufa Victor Kabulemi alisema hatua kubwa zilikuwa zimepigwa katika kuhakikisha hali ya usalama inarejea maeneo hayo, na kwamba matukio ya hivi karibuni yanavunja moyo.


Alisema tume hiyo inaendeleza uchunguzi kubaini kiini cha kuchipuka upya kwa uvamizi huu aliosema umepelekea vifo vya takriban wakazi 8 katika muda wa miezi miwili iliyopita, kisa cha hivi punde kikihusisha mauaji ya mama mjamzito eneo la Ramos.