Idara ya usajili yapelekea huduma ya vitambulisho mashinani Pokot Magharibi

Na Angela Cherono,
Idara ya usajili wa watu nchini inaendeleza zoezi la kuwasajili wakazi maeneo ya mashinani katika kaunti za maeneo kame nchini ambao wametimu umri wa kupata vitambulisho vya kitaifa ili wapate stakabadhi hizo.


Akizungumza wakati akiongoza zoezi hilo eneo la Soak kaunti ya Pokot magharibi, mkurugenzi wa idara ya usajili wa watu nchini Simon Karinge alisema wengi wa wakazi kutoka maeneo haya hawajakuwa wakipata huduma muhimu kutokana na kutokuwa na vitambulisho vya kitaifa.


Aidha Karinge alisema imekuwa vigumu kwa wakazi wa maeneo hayo kupata vitambulisho kutokana na ubovu wa miundo msingi na gharama inayoambatana na huduma hiyo.


“Tumeanza zoezi hili kwa sababu watu wetu katika maeneo haya hawajakuwa wakipata huduma kutokana na ukosefu wa vitambulisho. Wengi wao pia wamepata ugumu wa kupata vitambulisho kutokana na changamoto za barabara na pia gharama ya usafiri hadi afisi za usajili,” alisema Karinge.


Kauli yake ilisisitizwa na afisa wa usajili wa watu kaunti hiyo Carolyn Abwaku ambaye aidha alielezea changamoto wanazopitia kuwasajili wakazi kupata vitambulisho, akielezea haja ya kuendeshwa elimu ya umma kuhusu wanachohitajika kufanya wakazi kupata stakabadhi hiyo.


“Wengi wa wakazi maeneo haya hawafahamu kinachohitajika ili kupata vitambulisho. Tunahitaji kuendesha elimu ya umma ili kuwafahamisha wakazi umuhimu na kile ambacho wanahitaji kupata stakabadhi hii,” alisema Bi. Abwaku.


Wakazi wa eneo hilo wakiongozwa na aliyekuwa Chifu Simon Ng’oleruk walipongeza idara ya usajili kwa kupeleka zoezi hilo maeneo ya mashinani wakisema wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kupata stakabadhi hiyo kutokana na gharama ya usafiri hadi afisi husika.


Tunashukuru serikali kwa kutuletea zoezi hili hapa. Watu wetu wamekuwa wakikabiliwa na ugumu wa kusafiri hadi katika afisi ya usajili kupata vitambulisho kutokana na umbali na pia changamoto ya kupata gharama,” alisema Ng’oleruk.