Huenda ODM ikajiondoa Azimio kuelekea uchaguzi wa 2027; Poghisio

Samwel Moroto aliyekuwa seneta wa kaunti ya pokot Magharibi ,Picha/Maktaba

Na Emmanuel Oyasi,
Kuna uwezekano mkubwa wa chama cha ODM kuunda muungano mmoja na serikali ya Kenya kwanza kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.


Haya ni kwa mujibu wa aliyekuwa seneta wa kaunti ya Pokot magharibi Samwel Poghisio ambaye amesema uchaguzi mkuu ujao utashuhudia mirengo miwili pekee ikimenyana katika juhudi za kutwaa uongozi wa taifa.

Akizungumza katika mahojiano ya kipekee na kituo hiki, Poghisio alisema huenda chama cha ODM kikajiondoa kabisa katika mrengo wa azimio la umoja na kuunda muungano na Kenya kwanza, huku azimio ukishuhudia ujio wa viongozi wapya akiwemo aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua.


“Siasa za mwaka 2027 zimeanza kujipanga na naona kutakuwa na makundi mawili pekee yatakayokutana katika uchaguzi huo, kundi ambalo limesalia katika azimio na kundi litakaloundwa baada ya chama cha ODM kujiunga na Kenya kwanza,” alisema Poghisio.


Aidha Poghisio alisema huenda usuhuba wa karibuni kati ya rais William Ruto na kinara wa chama cha ODM Raila Odinga ukapelekea kubuniwa afisi mpya serikalini ambayo atahudumu Raila, katika juhudi za kuhakikisha kwamba uhusiano kati ya wawili hao unadumu kuelekea uchaguzi mkuu ujao.


“Huenda afisi mpya ikaundwa katika serikali ya Kenya kwanza, labda ya waziri mkuu ili Raila ahudumu serikalini katika juhudi za kuhakikisha kwamba uhusiano baina ya Raila na rais Ruto unaendelea kuimarika kuelekea uchaguzi mkuu ujao,” alisema.