Gavana Kachapin awafokea wanasiasa wanaoingilia utendakazi wa serikali yake

Na Emmanuel Oyasi,
Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin amewataka wanasiasa kuendeleza shughuli zao za kisiasa kwa uadilifu na kutoingilia utendakazi wa maafisa wa umma.


Akizungumza katika hafla moja mjini Kapenguria, Kachapin alisema serikali yake imezipa uhuru sekta mbali mbali kutekeleza majukumu yake bila ya miingilio, hali ambayo imeimarisha huduma ambazo zinatolewa na sekta hizo.

“Sekta za umma zinapasa kupewa uhuru wa kutekeleza kazi zake bila ya miingilio ya siasa. Mimi nimekuwa nikifanya hivyo. Siingilii sekta yoyote katika serikali yangu. Kwa hivyo tabia ya kuingiza siasa mahali ambapo hapatakikani ndio inarudisha nyuma maendeleo,” alisema gavana Kachapin.


Kauli yake ilisisitizwa na naibu wake Robert Komole ambaye alisema kuingiza siasa katika sekta za umma hakuhitilafiani tu na serikali iliyopo bali pia kuumiza wananchi kwa ujumla ambao mara nyingi hukosa huduma zinazohitajika.

“Nawahimiza viongozi wote, tusifanye siasa kuwa ni kitu cha kuwaumiza wakazi wa kaunti ya Pokot magharibi, tunapasa kufahamu kwamba watu wanaoajiriwa ni watoto wetu,” alisema Komole,”


Kwa upande wake mgombea ugavana wa kaunti hiyo, seneta wa zamani Samwel Poghisio aambaye alihudhuria hafla hiyo aliuhimiza uongozi uliopo kusalia imara katika kuwahudumia wananchi, na kutobabaishwa na pingamizi za wapinzani wake.


“Daima utakumbana na changamoto katika maswala muhimu katika uongozi wako. Hata sasa ukijaribu kufanya kitu kizuri, kuna mtu ambaye hafurahii. Lakini salia imara, hakuna haja ya kubabaishwa na mtu yeyote,” alisema Poghisio.