Chanjo ya HPV yazinduliwa wazazi wakihimizwa kuhakikisha wanao wanapewa chanjo hiyo

Na Benson Aswani,
Kundi la wake wa magavana nchini limetoa wito kwa wananchi kukumbatia chanjo ya kuzuia saratani ya kizazi HPV ambayo imezinduliwa rasmi na kundi hilo la wake wa magavana katika hafla iliyoandaliwa mjini Makutano kaunti ya Pokot magharibi.


Mwenyekiti wa kundi hilo mkewe gavana wa kaunti ya Marsabit Alamitu Jattani alisema saratani ya kizazi ni moja ya aina ya saratani ambazo zimewaangamiza kina mama wengi, na ni jukumu la wazazi kukumbatia chanjo ya HPV kwa ajili ya watoto wao wa kike ili kuzuia uwezekano wa kupata saratani hiyo.


“Saratani ya njia ya uzazi imeweza kuwaua kina mama wengi nchini. Lakini mtoto anapopata chanjo hii anakuwa na nafasi kubwa ya kutopata saratani hii. Kwa hivyo tunawaomba wazazi wahakikishe kwamba wanao wa kike wanapata chanjo hii,” alisema Bi. Jattani.


Kauli yake ilisisitizwa na mkewe gavana wa kaunti hii ya Pokot magharibi Bi. Scovia Kachapin ambaye aliwataka wakazi wa kaunti hiyo kupuuza dhana kwamba huenda wanaopata chanjo hiyo wakakosa kupata watoto, akiwahakikishia kwamba imethibitishwa kuwa ni salama.


“Katika kaunti hii kuna imani kwamba mtu anapopata chanjo hii hawezi kupata watoto baadaye. Lakini nawahakikishia watu wetu kwamba chanjo hii ni salama na imethibitishwa,” alisema Bi. Scovia.


Kwa upande wake mtaalam wa afya ya kina mama Dkt. Nelly Bosire alitoa hakikisho kwa wakazi wa kaunti hiyo kwamba chanjo hiyo si mpya kwani imekuwa ikitumika kwa muda wa miaka 20 iliyopita.


“Hii chanjo imekuwepo kwa miaka mingi na si chanjo ngeni. Ni vile tu kwa sababu taifa letu halijajiweza sana kiuchumi, ndio maana imechukua muda mrefu kupata chanjo hii kuwapa watoto nchini,” alisema Dkt. Bosire.