Lomunokol aandikisha taarifa na DCI kufuatia matamshi ya uchochezi,

Na Benson Aswani,
Aliyekuwa mbunge wa kacheliba kaunti ya Pokot Magharibi Mark Lomunokol amewasuta baadhi ya wanasiasa kaunti hiyo kwa kile amesema kutumia mbinu potofu kumpiga vita vya kisiasa hasa wakati huu ambapo uchaguzi mkuu unakaribia.


Akizungumza baada ya kurekodi taarifa katika kituo cha polisi cha kapenguria kufuatia matamshi aliyotoa eneo la Soka, ambayo yanadaiwa kuwa ya uchochezi, Lomunokol alisemasema alinukuliwa visivyo na mahasimu wake wa kisiasa kwa lengo la kumchafulia jina.


Alitoa wito kwa idara za uchunguzi kutokubali kutumika kisiasa dhidi ya viongozi wengine wa kisiasa na badala yake kutekeleza majukumu yake kulingana na taratibu za kisheria.

“Nimerekodi taarifa na maafisa wa polisi kufuatia kauli niliyotoa eneo la Soka ambayo ilichukuliwa vibaya na baadhi ya viongozi katika kaunti hii. Nadhani kuna watu ambao wana nia mbaya ya kuniharibia sifa machoni pa wananchi,” alisema Lomunokol.


Ni kauli ambayo ilisisitizwa na mbunge wa sigor Peter Lochakapong aliyeandamana naye katika kituo hicho cha polisi, na ambaye alidai ni njama iliyopangwa, akimlaumu gavana wa kaunti hiyo Simon Kachapin kwa masaibu hayo ambayo yanamwandama Lomunokol.


Lochakapong alidai gavana Kachapin aliahidi awali kutuma rekodi ya maneno yanayodaiwa kutolewa na Lomunokol kwa idara za uchunguzi.


“Gavana Simon Kachapin aliahidi kutuma sauti aliyodai kwamba ilikuwa na ujumbe wa uchochezi kwa maafisa wa DCI ili wamfanyie uchunguzi Lomunokol. Na hakika imetimia. Mimi nataka tu kuwaambia maafisa hawa kwamba watekeleze majukumu yao kwa usawa na kutoruhusu kushinikizwa na baadhi ya wanasiasa,” alisema Lochakapong.