Mgomo wa wauguzi wasitishwa Pokot magharibi

Na Benson Aswani,
Huduma za matibabu zinatarajiwa kurejelewa rasmi katika kaunti ya Pokot magharibi baada ya kuysitsihwa rasmi mgomo wa wauguzi ambao umekuwa ukiendelea kwa wiki ya sita sasa.


Gavana wa kaunti hiyo Simon Kachapin alifanya kikao jumatatu tarehe 8 mwezi Septemba na wakuu wa muungano wa maafisa hao KUCO na kuafikia makubaliano ya kutekeleza mkataba wa maelewano na uongozi wa muungano wa maafisa hao, mazungumzo aliyosema yamekuwa yakiendelea kwa muda sasa.


Gavana Kachapin alipongeza kusitishwa kwa mgomo huo, hatua aliyosema ni afueni kubwa kwa wakazi ambao wamekuwa wakipitia wakati mgumu kupata huduma za matibabu.


“Nimefurahi leo kwa sababu tumekuwa na mazungumzo, na si mazungumzo ambayo yameanza leo. Ni mazungumzo ambayo yamekuwa yakiendelea kwa muda, na tumekubaliana kuhusu mambo kadhaa ambayo sisi kama serikali tunapasa kutekeleza,” alisema Gavana Kachapin.


Aidha gavana Kachapin aliahidi kuwa uongozi wake utahakikisha makubaliano ya kurejea kazini ambayo yameafikiwa baina yake na maafisa hao wa afya yanatekelezwa kikamilifu ili wakazi wasipitie tena mahangaiko ya kukosa huduma za matibabu.


“Kama serikali ya kaunti, tunaahidi kuhakikisha kwamba tunatekeleza kikamilifu mambo ambayo tumekubaliana leo, ili watu wetu wasihangaike tena kupata huduma za matibabu kwa sababu ya migomo,” alisema.


Kwa upande katibu mkuu wa kitaifa wa muungano huo George Gibore alisema kaunti ya Pokot magharibi sasa imejiunga na kaunti zingine ambazo tayari zimeafikiana kutekeleza makubaliano hayo.


“Tunafurahi sana kwamba sasa mvutano ambao umekuwepo baina ya wahudumu wa afya na serikali ya kaunti umetatuliwa. Na kaunti ya Pokot magharibi sasa inakuwa miongoni mwa kaunti ambazo zimeafikia kutekeleza makubaliano ambayo yalikuwepo na wahudumu hawa wa afya,” alisema Gibore.


Aliwataka wahusika kuhakikisha swala la marupurupu hasa kwa maafisa walio kwenye mpango wa UHC linatekelezwa kikamilifu.