Kachapin aahidi kuimarisha hali ya Pokot Magharibi kabla ya kuondoka afisini

Na Benson Aswani,
Gavana wa kaunti ya Pokot Magharibi simon kachapin amesema serikali yake inawekeza katika ujenzi wa taasisi za elimu pamoja na miundombinu ili kufungua zaidi kaunti hiyo kwa wakenya na kuboresha taswira ya eneo hilo.
Kulingana na gavana kachapin kaunti hiyo imewekeza katika taasisi za elimu ikiwemo chuo cha utabibu, KMTC, chuo cha elimu ya awali ECDE, taasisi ya mafunzo ya walimu, TTC pamoja na chuo kikuu cha Kapenguria.
Gavana kachapin alisema uwepo wa taasisi hizo utawapa wanafunzi wa Pokot Magharibi nafasi ya kupata elimu ya juu karibu nao, huku pia ukiwavutia wanafunzi kutoka maeneo mengine ya nchi.
“Kaunti yetu haina chuo kikuu hata kimoja. Mimi nikaamua nikasema hata kama tutasubiri serikali ya kitaifa, sisi wenyewe kupitia raslimali zetu kidogo tuweke chuo cha mafunzo ya udaktari KMTC pale Kapenguria na chuo cha mafunzo ya walimu TTC pale Chester,” alisema Kachapin.
Aidha gavana huyo alisema serikali ya kaunti pia inaendelea kuboresha miundombinu, ikiwemo barabara na taa za barabarani, ili kuwezesha maendeleo na kuboresha huduma kwa wananchi.
Kachapin aliongeza kuwa uwekezaji katika elimu, miundombinu na taasisi mbalimbali ni miongoni mwa njia za kuiwezesha Pokot Magharibi kufunguka zaidi na kujenga fursa kwa wananchi.
“Barabara zetu bado ni mbaya lakini tumejaribu. Hakukuwa na taa za barabarani hata moja ila sasa tumeweka, na mimi najua tukiendelea hivyo mambo yatakuwa mazuri,” alisema.
