Kachapin awataka wahudumu wa afya kurejea kazini

Na Benson Aswani,
Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin ametoa wito kwa wahudumu wa afya ambao wanaendeleza mgomo wao kuyapa nafasi mazungumzo ili kupata suluhu ya jinsi ya kushughulikia matakwa yao.
Akizungumza katika hafla moja eneo la Bendera, gavana Kachapin alisema inasikitisha kuona kwamba wagonjwa wanaendelea kukosa huduma muhimu za afya kwa maswala ambayo yangesuluhishwa kupitia mazungumzo.
Kachapin alikiri kwamba yapo maswala ambayo hayajatimizwa katika mkataba wao wa makubaliano, ila akawasihi wahudumu hao kulegeza kamba na kushiriki mazungumzo, akitoa hakikisha la kutekelezwa maswala ambayo wahudumu hawa wanashinikiza.
“Nataka niwahakikishie wahudumu wetu wa afya kwamba mambo machache ambayo hayajatimizwa na serikakli ya kaunti yatatimizwa. Kile ninawaomba ni kwamba, tuweke mazungumzo mbele kwa sababu mgomo hautasuluhisha kiti chochote, ila ni wagonjwa wanaoendelea kuumia,” alisema gavana Kachapin.
Kando na hayo gavana Kachapin alielezea kuunga mkono ruwaza ya mwaka 2060 iliyowasilishwa kwa taifa na rais William Ruto siku chache zilizopita, akisema itasaidia pakubwa taifa kupiga hatua kimaendeleo na kufikia mataifa yaliyostawi kiuchumi.
“Mimi naunga mkono ruwaza aliyozindua rais ya mwaka 2060. Si makosa kuwaza mambo mazuri. Nchi yoyote ambayo inaendelea ni lazima iwe na maono ya hapo mbele,” alisema.
