Poghisio adokeza kuhusu uwezekano wake kufanya kazi na gavana Kachapin katika serikali ijayo

Na Benson Aswani,
Aliyekuwa seneta wa kaunti hii ya Pokot Magharibi Samwel Poghisio ameendelea kujipigia debe katika azma yake ya kuwania ugavana wa kaunti hiyo katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.


Akizungumza katika ibaada ya jumapili kwenye kanisa la full gospel Chepareria, Poghisio alisema yeye ndiye anayefaa kuongoza kaunti hiyo kutokana na tajriba yake katika kipindi ambacho amehudumu katika ulingo wa kisiasa.

Aidha alidokeza kwamba huenda wakahudumu na gavana wa sasa Simon Kachapin katika serikali ijayo iwapo atachaguliwa gavana, ambapo gavana Kachapin atahudumu kama seneta wakati atakapohitimisha kipindi chake cha ugavana kaunti hiyo.


“Mimi na gavana wa sasa tunatosha kuwa pamoja katika serikali ijayo, mimi nikiwa gavana na yeye akiwa seneta. Leo katika jukwaa hili ni mimi peke yangu ndiye naomba kiti cha ugavana. Hakuna upinzani. Na mimi ndiye mwanasiasa mwenye tajriba katika kaunti hii,” alisema Poghisio.


Poghisio aliwahimiza wakazi wa kaunti hiyo kuzingatia viongozi ambao watawachagua katika uchaguzi mkuu ujao akiwataka kujitenga na viongozi aliowataja kuwa wasio na heshima kwa matamshi yao dhidi ya viongozi wengine.


“Nawaomba watu wetu katika kaunti hii, tujitenge kabisa na wanasiasa ambao wanatusiana kila wakati. Kuna makundi ambayo wanapigana na kutusiana, na tuwe makini na watu tutakaowachagua,” alisema.


Ikumbukwe gavana wa sasa katika kaunti hiyo Simon Kachapin alidokeza kwamba atatangaza mwelekeo wake wa kisiasa mwezi Agosti baada ya hatamu yake ya ugavana kumalizika mwaka ujao.