Bodi simamizi ya hospitali ya Kapenguria yafanyiwa mabadiliko ya uongozi

Na Benson Aswani,
Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin ameendelea kusifia ugatuzi akisema umepelekea maendeleo mengi ambayo hayakushuhudiwa katika serikali za awali.
Akizungumza wakati wa kuteuliwa uongozi mpya wa bodi simamizi ya hospitali za Kapenguria, Kacheliba, Chepareria na Sigor, gavana Kachapin alisema kupitia ugatuzi, idara muhimu kama vile ya afya zimeimarika pakubwa.
“Lengo kuu la ugatuzi lilikuwa kuboresha huduma kwa wananchi. Na mimi kama gavana nafurahi kwa sababu tumepiga hatua hasa katika idara ya afya,” alisema Gvn. Kachapin.
Gavana Kachapin aliahidi kushirikiana na bodi mpya ya hospitali hizo kwa kubuni mazingira bora ya utendakazi wake, ili kuhakikisha kwamba inatoa huduma bora ambazo zitaimarisha zaidi sekta ya afya katika kaunti hiyo.
“Tutashirikiana pakubwa na bodi hii mpya kwa kuhakikisha kwamba inapata mazingira bora ya kutekeleza shughuli zake ili kuimarisha huduma za afya kwa wakazi wa kaunti hii ya Pokot magharibi,” alisema.
Mwenyekiti wa bodi hiyo anayeondoka Dkt. Philip Parklea alisifia hatua ambazo zimepigwa katika uongozi wake wa mihula miwili ya bodi hiyo, juhudi ambazo mwenyekiti anayeingia Charles Alsereng aliahidi kuendeleza.
“Kwa huu muda ambao tumesimamia bodi hii tumeweza kuimarisha hospitali hizi, kwa mfano wagonjwa walikuwa wakitumwa sana katika hospitali za nje ya kaunti kufuatia kukosekana baadhi ya huduma, lakini sasa huduma nyingi zinapatikana katika hospitali zetu na sasa wagonjwa hawalazimiki kutafuta huduma hizo nje,” alisema Dkt. Parklea.
