Serikali ya kitaifa yaipa msaada shule ya msingi ya Nasokol kufuatia mkasa wa moto
Na Benson Aswani
Shule ya msingi ya Nasokol eneo bunge la Kapenguria katika kaunti ya Pokot magharibi imepokea msaada kutoka kwa serikali kuu kufuatia mkasa wa moto ambao uliteketeza mabweni mawili pamoja na mali ya wanafunzi takriban miezi miwili iliyopita.

Akizungumza wakati akipokea msaada huo unaojumuisha chakula na vifaa mbali mbali, afisa wa uhakiki wa ubora katika idara ya elimu eneo bunge la Kapenguria Philemon Rop, alisema hatua hiyo inakusudiwa kuhakikisha shule hiyo inarejea katika nafasi yake ya awali kabla ya mkasa huo wa moto, akiipongeza serikali ya kitaifa kwa msaada huo.
“Shule hii imekuwa shule nzuri, imekuwa kifanya vyema na wakati mkasa huu ulipotokea, sisi kama idara ya elimu tulihuzunika sana. Lakini tunashukuru sasa kwa vile serikali ya kitaifa imekuja kuisaidia shule hii kurejea mahali pake pa awali,” alisema Rop.
Msaidizi wa kamishina eneo bunge la Kapenguria Peter Njuguna alisema serikali imeweka mikakati mwafaka ikiwemo kuandaa vikao na wadau mbali mbali kuhakikisha kwamba mkasa kama huu haushuhudiwi tena shuleni.
“Tumekuwa na mikutano mingi ya kujaribu kuongea na walimu wakuu pamoja na wadau wengine ikiwemo wanafunzi, katika juhudi za kuhakikisha kwamba tunazuia visa kama hivi kushuhudiwa siku za usoni,” alisema Njuguna.
Uongozi wa shule hiyo ukiongozwa na mwalimu mkuu Cecilia Ngige ulipongeza serikali na wahisani mbali mbali kwa msaada ambao walipokea akisema utasaidia pakubwa kupoza makovu yaliyosababishwa na mkasa huo wa moto.
“Hii misaada itasaidia pakubwa wanafunzi kurejelea hali yao ya kawaida. Na nishukuru kwamba, licha ya kwamba tulikuwa na mkasa huo wa moto, masomo yaliendelea kama kawaida, na hatukutatizika,” alisema Bi. Ngige
