Serikali yaahidi mazingira bora kwa wafanyibiashara Pokot Magharibi

Na Emmanuel Oyasi,
Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin amesisitiza dhamira ya serikali ya kaunti ya kuhakikisha kuna mazingira bora kwa wafanyabiashara kupitia uboreshaji wa miundombinu, sera zinazounga mkono biashara na ushirikiano wa karibu kati ya sekta ya umma na binafsi.
Akizungumza katika mkutano na wadau kwenye sekta ya biashara, gavana Kachapin alisema wafanyibiashara ni nguzo muhimu kwa uchumi wa kaunti, na ni jukumu la serikali kufahamu changamoto ambazo zinawakabili na kuhakikisha suluhu inapatikana katika juhudi za kuimarisha uchumi.
“Biashara ndiyo nguzo kubwa ya uchumi wa kaunti, na wale ambao wanasukuma uchumi wetu ni lazima tuwatambue, kupitia kujadiliana na wafanyibiashara ili tujue wanapitia changamoto gani, na jinsi tunavyoweza kuwasaidia katika biashara zao,” alisema Kachapin.
Aidha, gavana Kachapin alisema serikali yake imekamilisha maandalizi ya mkutano mkubwa wa uwekezaji utakaofanyika mwezi Agosti mwaka huu, akisema kongamano hilo linalenga kuvutia wawekezaji kutoka maeneo mbalimbali nchini na nje ya nchi.
Kulingana naye, mkutano huo utatoa jukwaa kwa wafanyabiashara na wawekezaji kutangaza biashara zao huku ukitoa fursa ya kuangazia rasilimali mbalimbali zilizopo katika kaunti ya pokot magharibi.
“Tuna lengo la kuandaa kongamano kubwa la uwekezaji mwezi Agosti ambalo tuna imani litakuwa lenye umuhimu mkubwa kwa wafanyibiashara na kaunti kwa ujumla, ikizingatiwa raslimali nyingi ambazo tunajivunia kaunti hii,” alisema.
