Baa la njaa lawakodolea macho wakazi wa pokot kaskazini

0-4480×2038-0-0#

Na Benson Aswani,
Serikali ya taifa hili na taifa jirani la Uganda zimetakiwa kuanza mikakati ya kuhakikisha wakazi wa maeneo ya Pokot kaskazini kaunti ya Pokot magharibi na Amudat katika taifa jirani la Uganda wanapata chakula cha msaada mwaka ujao.


Ni wito ambao umetolewa na mbunge wa Upe katika Wilaya ya Amudat Micah Lobang’ang, ambaye alisema maeneo hayo yameathirika pakubwa na kiangazi ambacho kinaendelea kushuhudiwa kwa sasa.


Akizungumza eneo la Konyao kaunti ya Pokot Magharibi, Lobang’ang alimtaka rais William Ruto na mwenzake wa Uganda Yoweri Museveni kushirikiana na kuhakikisha kwamba wakazi wa eneo hilo hawapitii mahangaiko kutokana na baa la njaa ambalol linatarajiwa.


“Hakuna mahindi huku. Kiangazi ambacho kimeshuhudiwa maeneo haya kimewapelekea wakulima hasara kubwa. Kwa hivyo ni jukumu la serikali ya Kenya na Uganda kuweka mikakati itakayohakikisha kwamba wakazi wa maeneo haya wanapata chakula,” alisema Lobang’ang.

Wakati uo huo Lobang’ang aliwataka viongozi wa mataifa haya mawili kuanzisha miradi ya unyunyiziaji maji mashamba maeneo haya ili wakazi waendeleze kilimo bila kuhitilafiwa na uchache wa mvua ambao umekuwa ukishuhudiwa kwa muda sasa.


“Kwa sababu haitakuwa bora kwa wakazi wa maeneo haya ya Pokot kaskazini na Amudat kutegemea serikali kwa chakula kila mwaka, tunapasa kuweka mikakati ya muda mrefu kupitia miradi ya unyunyiziaji maji mashamba ili wakazi wasipate matatizo kufuatia uchache wa mvua,” alisema.