Poghisio: Lazima tujitenge na chuki za kisiasa na tuwahudumie wananchi

Na Emmanuel Oyasi,
Aliyekuwa seneta wa kaunti ya Pokot magharibi dkt Samwel Poghisio ameshutumu vikali hulka ya magavana wanaokuja mamlakani kutelekeza miradi ambayo ilikuwa ikitekelezwa na watangulizi wao.


Dkt Poghisio ambaye ametangaza nia ya kuwania ugavana wa kaunti hiyo kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka ujao, alisema hulka hiyo haistahili kwani inapelekea kupotea fedha nyingi za walipa ushuru ambazo tayari ziliwekezwa kwenye miradi hiyo.

Alisema iwapo atachaguliwa kuongoza kaunti hiyo kwenye uchaguzi ujao ataipa kipau mbele miradi ambayo ilianzishwa na serikali iliyopo na ambayo bado haijakamilishwa, kabla ya kuanza miradi mipya ili iwafaidi wananchi na kuhakikisha fedha za walipa ushuru zinatumika vyema.


“Chuki iliyopo katika siasa ni mbaya sana. Kwa sababu gavana ambaye anakuja anaacha kazi za gavana mwenzake ambaye alimtangulia na anaanza zingine na pesa ni zilezile tu ambazo zinakuja katika kaunti.

Ni lazima kwanza tumalize ile miradi ambayo haikukamilika kwa sababu pesa zake bado zipo kwenye bajeti,” alisema Poghisio.


Wakati uo huo dkt Poghisio ambaye aliwahi kuhudumu kama kiongozi wa wengi katika bunge la seneti aliapa kuhakikisha kwamba madeni yanayodaiwa na wanakandarasi waliotoa huduma kwa serikali ya kaunti, yanalipwa ili kuendeleza uhusiano mwema na wadau wote.


“Katika bajeti yangu ya kwanza nitahakikisha kwamba madeni ya wale watu ambao walifanya kazi na kaunti yanalipwa. Sitaki kuwa serikali ambayo inaumiza wafanyibiashara,” alisema.