Wakazi Pokot magharibi waiomba serikali kuwapa pembejeo za kilimo

Na Emmanuel Oyasi
Wito umetolewa kwa serikali ya kaunti ya Pokot magharibi chini ya gavana Simon Kachapin kuendeleza mpango wa kugawa mbegu na mbolea kwa wakazi hasa maeneo ya mashinani ambao hawana uwezo wa kununua pembejeo hizo hasa msimu huu wa upanzi.


Akizungumza na wanahabari, aliyekuwa mwakilishi wadi Teresa Lokichu alisema wapo wengi wa wakazi ambao wameshindwa kuendeleza shughuli ya kilimo licha ya kuanza msimu wa upanzi, na ingekuwa bora iwapo serikali ya kaunti ingechukua jukumu la kuwapiga jeki.

“Mbolea na mbegu hazijafika huku maeneo ya mashinani. Tunamwomba gavana kuhakikisha kwamba anatuletea mbegu na mbolea hasa kwa wazee, kina mama wajane na wakazi ambao hawana uwezo wa kuzinunua, ili pia waweze kutumia msimu huu wa mvua kupanda,” alisema Lokichu.


Aidha, Lokichu alielezea haja ya kuwekwa maghala ya kusambaza mbolea ya ruzuku maeneo ya mashinani, akisema wengi wa wakulima wanapata wakati mgumu kusafiri hadi mjini Makutano kununua mbolea hiyo kufuatia gharama kubwa ya usafiri.

“Kwa sasa hakuna mbolea ambayo imefika mashinani. Watu wanangojea, mvua ndio hii imenyesha, lakini hakuna mbolea imefika. Makutano ni mbali na ni vigumu kwa watu kutoka mashinani kufika kuchukua mbolea kwa sababu ya gharama ya usafiri,” alisema.


Kauli yake ilisisitizwa na baadhi ya wakazi wa kaunti hiyo ambao walielezea hofu kwamba huenda msimu wa upanzi ukakamilika kabla ya wao kupanda kutokana na kutokuwa na uwezo wa kununua pembejeo hizo.