Gavana Kachapin atia saini mswada wa kukabili umasikini Pokot magharibi

Na Benson Aswani,
Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin ametia saini kuwa sheria mswada utakaoiwezesha serikali ya kaunti kutenga kisheria fedha ambazo zitasaidia katika kuimarisha maisha ya wakazi wa kaunti hiyo walio chini kiuchumi, maarufu Poverty Graduation Bill.
Akizungumza na wanahabari baada ya kutia saini mswada huo, gavana Kachapin alisema hatua hii ni katika harakati za kutimiza ajenda yake ya kuhakikisha anakabiliana na swala la umasikini, ikiwa ni moja ya ahadi ambazo alitoa kwa wakazi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita.
“Kaunti yetu ya Pokot magharibi kupitia hii sheria itaweza kutenga fedha kuwezesha wale ambao wapo chini, wainuliwe ili kupunguza umasikini ambao unawakumba watu wetu. Hatua hii inaendana na manifesto yangu ambapo nilisema ni lazima tupambane na umasikini ambao umekita katika jamii yetu,” alisema gavana Kachapin.
Gavana Kachapin aliipongeza wizara ya utamaduni, utalii, michezo, vijana na huduma za kijamii chini ya waziri Lucky Litole, na bunge la kaunti pamoja na washirika wote kwa kuhakikisha kwamba mchakato huo unafanikishwa kwa manufaa ya wakazi wa kaunti hiyo.
“Nataka nishukuru wizara ikiongozwa na waziri Lucky Litole na timu yake, na bunge la kaunti kwa kazi nzuri ambayo imetufikisha leo ambapo nimetia saini hiyo sheria,” alisema.
Kwa upande wake waziri Litole alisema kutakuwa na mfumo utakaosaidia kubaini wakazi ambao wanafaa kulingana na viwango vyao vya umasikini, ambapo kando na kupewa fedha, watapewa pia mafunzo ya jinsi ya kuanzisha biashara.
“Kuna mfumo tutakaotumia kuwapata wakazi ambao wanastahili kulingana na viwango vya umasikini ili tuwape mtaji wa kuanza biashara. Kando na kuwapa tu fedha, pia watapata mafunzo ambayo yatawasaidia katika kuanzisha biashara hiyo,” alisema Litole.
