Serikali ya Kenya kwanza imejitolea kuimarisha maisha ya mwananchi; Arumonyang

Na Benson Aswani,
Katibu wa idara ya kazi za umma Joel Arumonyang ametetea miradi ya maendeleo ambayo inaendelezwa na serikali yake rais William Ruto, akisema serikali kuu imejitolea kuimarisha maisha ya mwananchi.


Akizungumza katika afisi za gavana wa kaunti ya Pokot magharibi, Arumonyang alisema miradi kama vile ujenzi wa nyumba za bei nafuu imesaidia pakubwa kubuni ajira kwa vijana ambao wamehusishwa kikamilifu kwenye mradi huo.

Aidha Arumonyang alisema serikali imejitolea kuboresha viwango vya elimu kupitia kuwaajiri walimu zaidi akisema kufikia sasa serikali ya rais William Ruto imewaajiri walimu zaidi ya alfu 100.


“Moja ya ajenda za serikali yetu ni kubuni nafasi za ajira. Unaweza kuona kwamba, sasa mradi ya ujenzi wa nyumba za bei nafuu umeweza kuwaajiri vijana wengi. Lengo letu ni kuhakikisha kwenda mbele tunainua maisha ya wananchi,” alisema Arumonyang.


Wakati uo huo Arumonyang alitoa wito wa kusambazwa mbolea ya ruzuku hadi maeneo ya mashinani akisema wengi wa wakulima wanakabiliwa na wakati mgumu na hata kulazimika kugharamika zaidi kufika mjini makutano kununua mbolea hiyo kwenye maghala ya NCPB.


“Swala moja ambalo ningependa kutaja ni usambazaji wa mbolea katika kaunti hii, kwa kuwa mimi ni mkulima na naelewa changamoto zilizo hapa. Hili ghala la hapa lipo mbali sana. Kungewekwa maghala mengine sehemu za mashinani ambapo wakazi wataweza kupata mbolea bila kugharamika zaidi kufika mjini Makutano,” alisema.