Zoezi la kutwaa silaha haramu bonde la kerio linaendelea vyema; Murkomen

Na Benson Aswani,
Waziri wa usalama na maswala ya ndani ya nchi Kipchumba Murkomen ameelezea imani kwamba zoezi la kutwaa silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria na baadhi ya wakazi wa kaunti za Bonde la Kerio litafanikisha juhudi za kuafikia usalama katika kaunti hizo.
Akizungumza mjini Makutano kaunti ya Pokot magharibi wakati wa uzinduzi wa zoezi la kuwasajili wakazi wasio na vitambulisho vya kitaifa kupokea stakabadhi hizo muhimu, Murkomen alisema vikosi vya usalama vimeendelea kupokea silaha ambazo zinasalimishwa na wakazi kwa hiari.
Aidha Murkomen alisema wizara hiyo inalenga kuanza awamu nyingine ya kutwaa silaha hizo mpakani pa kaunti ya Pokot magharibi na kaunti jirani ya Turkana ambako kumekuwa kukishuhudiwa uvamizi wa mara kwa mara.
“Tumekuwa tukiendesha oparesheni ya kiusalama kutwaa silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria kati ya Pokot magharibi na Elgeyo Marakwet, na Elgeyo marakwet na Baringo, na zoezi hilo linaendelea vyema, hata jana tuliweza kupokea bunduki 20. Sasa tunataka kuelekeza zoezi hilo kwenye mpaka wa Pokot magharibi na Turkana,” alisema Murkomen.
Murkomen alisema silaha bado zinamilikiwa mpakani pa kaunti hizi kutokana na ukame ambao unaendelea kuhushuhudiwa, na baadhi ya wakazi wanalazimika kutumia silaha hizo katika kuwatafutia mifugo wao malisho na maji.
“Wengi wa wakazi eneo hili wanamiliki silaha haramu kutokana na ukame ambao umekithiri, ambapo wanazitumia kutafuta lishe na maji kwa mifugo, na hiyo ndiyo sababu tuta tatizo kati ya Pokot magharibi na Baringo na Pokot magharibi na Turkana,” alisema.
