Mwekezaji Salah Okech aanzisha mradi wa chakula kwa wakazi Songok

Na Benson Aswani,
Wakazi wa maeneo ambako kunaendelezwa shughuli ya uchimbaji madini kaunti ya Pokot magharibi wameendelea kunufaika na huduma ambazo zinatolewa na baadhi ya wawekezaji katika sekta hiyo maeneo hayo.
Hii ni baada ya mwekezaji Salah Okech kuanza mradi wa kupeana chakula mara mbili kwa mwezi kwa wakazi wa eneo hilo.
Akizungumza na wanahabari eneo la Songok wadi ya Kasei Okech alisema amechukua hatua hiyo ili kuwaepushia wakazi wa eneo hilo makali ya njaa kutokana na ukame ambao umekithiri.
Okech alisema tayari visima sita vya maji vimechimbwa maeneo hayo huku mradi wa chakula kwa wanafunzi ukiendelea.
“Mnavyojua tumechimba visima sita hapa vya maji kuwasaidia wakazi eneo hili, na pia tunapeana chakula kwa shule ili watoto wasipate changamoto ya kukabiliwa na hali ya njaa. Leo pia tumeanzisha mradi wa kuwapatia wakazi wa sehemu hii chakula mara mbili kwa mwezi,” alisema Okech.
Wakazi wa meneo hayo wakiongozwa na Joseph Domo walipongeza juhudi za mwekezaji huyo wanazosema zimekuja kwa wakati unaostahili ikizingatiwa hamna shughuli ya kilimo inayoendelea kutokana ukame ambao umekithiri.
“Tumefurahi kwa sababu sasa tumepata maji ambayo tumeomba kwa muda sana viongozi wetu watuletee, lakini Salah ametimiza ombi letu. Kwa hivyo kama jamii ya Songok tunashukuru sana,” alisema Domo.
