Kaunti ya Pokot Magharibi yapokea dawa za kima cha shilingi milioni 70 kutoka KEMSA

Na Benson Aswani,
Huduma za matibabu katika kaunti ya Pokot magharibi zinatarajiwa kuimarika baada ya kaunti hiyo kupokea dawa na vifaa vya matibabu vya kima cha shilingi milioni 70 kutoka kwa mamlaka ya kusambaza dawa na vifaa vya matibabu nchini KEMSA.
Akizungumza baada ya kupokea shehena ya dawa hizo, gavana wa kaunti hiyo Simon Kachapin alisema hicho ni kiwango cha juu zaidi cha dawa ambazo zimewahi kupokelewa na kaunti hiyo, akipongeza idara ya afya kwa kushirikiana na KEMSA kuhakikisha dawa hizo zinawasilishwa.
“Tumepokea dawa ya zaidi ya shilingi milioni 70 kutoka kwa KEMSA. Nashukuru sana idara ya afya kaunti hii kwa kuwajibika kwa wakati kwa kuwa hii ndiyo shehena kubwa zaidi ya dawa kuwahi kupokelewa kaunti hii ,” alisema gavana Kachapin.
Aidha, gavana Kachapin alipongeza mamlaka ya KEMSA kwa kuhakikisha kwamba dawa na vifaa vyote ambavyo viliagizwa na kaunti hiyo vinawasilishwa, hatua aliyosema inaashiria kuimarika zaidi utendakazi wa mamlaka hiyo.
“Nashukuru pia KEMSA kwa kuhakikisha kwamba dawa na vifaa vyote vya matibabu ambavyo tuliitisha vimewasilishwa. Hii ni ishara tosha ya kuimarika huduma za mamlaka hii,” alisema.
Wakati uo huo gavana Kachapin alitoa wito kwa usimamizi wa hospitali na vituo vya afya kaunti hiyo kuhakikisha kwamba dawa hizo zinatumika vyema, akitoa onyo kali kwa wahudumu wa afya ambao wamekuwa wakijihusisha na wizi wa dawa kwamba watakabiliwa kisheria pindi wakipatikana.
“Wale wanafanya kwa hospitali mbali mbali watumie hizi dawa vizuri. Natoa onyo kwa wale ambao watapatikana wakijihusisha na wizi wa dawa kwamba watachukuliwa hatua kali sana,” alisema.
