Viongozi Pokot magharibi na Turkana watakiwa kuimarisha mazingira ya kutekelezwa miradi ya maendeleo

Na Benson Aswani,
Waziri wa maswala ya afrika mashariki, maendeleo ya kikanda na maeneo kame Beatrice Askul amewataka viongozi wa kaunti za Pokot magharibi na Turkana kushirikiana kuhakikisha kwamba hali ya utulivu inaendelea kushuhudiwa maeneo ya mipaka ya kaunti hizo.
Akizungumza katika kikao cha ushauri na viongozi wa kaunti za Pokot magharibi na Turkana kilichoandaliwa eneo la Turkwel, Askul alisema visa vya utovu wa usalama mipakani pa kaunti hizo mbili umepelekea wawekezaji kuondoka na kupelekea maeneo haya kusalia nyuma kimaendeleo.
“Ni wakati ambapo viongozi eneo hili tunapasa kushirikiana kuhakikisha kwamba kunashuhudiwa amani kwa ajili ya watu tunaowaongoza. Eneo hili lina raslimali nyingi ila limesalia nyuma kwa sababu ya utovu wa usalama,” alisema Askul.
Askul vile vile, alisema uongozi wa rais William Ruto umeweka mikakati ya kuhakikisha kwamba wakazi wa maeneo hayo wanaboresha maisha yao kwa kutumia raslimali zilizopo, ikiwemo bwawa la Turkwel kwa kuendeleza miradi ya kilimo chini ya mradi wa the Lower Turkwel Irrigation Project.
“Hili sasa limeingia katika mawazo ya rais wetu kwamba tutumie raslimali ambazo Mungu ametupa ili kuboresha maisha ya watu wetu na kuimarisha maendeleo eneo hili,” alisema
Viongozi wa meneo hayo wakiongozwa na gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin na mwenzake wa Turkana Jeremiah Lomurkai walipongeza mradi huo waliosema utakuwa wenye manufaa makubwa katika kukabili tatizo la uhaba wa chakula.
Gavana Kachapin aliipongeza serikali ya rais William Ruto kwa kuweka mikakati ya kuhakikisha kwamba mradi huo wa zaidi ya ekari 3000 za ardhi unatekelezwa.
“Mambo ya unyunyiziaji maji mashamba ni faida kubwa kwa hawa wananchi. Na kama zaidi ya miaka 30 serikali zingine zote hazingeweza kutekeleza mradi huu, tunaishukuru serikali yetu ya Kenya kwanza kwa kuonyesha nia ya kuimarisha maisha ya watu wetu,” alisema Gavana Kachapin.
Kauli yake ilisisitizwa na gavana wa kaunti ya Turkana Jeremiah Lomurkai ambaye hata hivyo alisema asilimia kubwa ya mazao ambayo yatapatikana kwenye mradi huo yanapasa kusalia mikononi mwa jamii za maeneo husika.
“Asilimia 60 ya mazao ambayo yatatoka kwenye mradi huu lazima isalie mikononi mwa watu wa hapa. Hivyo ndivyo inavyopasa kuwa. Tunaunga kikamilifu ajenda ya rais kuhakikisha kwamba jamii ya wafugaji pia inaangazia kilimo,” alisema Gavana Lomurkai.
Kwa upande wake mwenyekiti wa bodi ya shirika la maji, kazi na maendeleo kaskazini mwa bonde la ufa, (North Rift Valley Water Works Development Agency) John Lonyangapuo alihimza ushirikiano miongoni mwa wadau ili kufanikisha mradi huo.
“Tunapoanza mambo ya unyunyiziaji maji mashamba, tuanze kwa ukweli. Serikali kuu na serikali za kaunti tusemezane sote tuone jinsi ambavyo tutaanza na kuendeleza mradi huu,” alisema Prof. Lonyangapuo.
