Wanafunzi 74 wanufaika na ufadhili wa elimu kupitia mpango wa Elimu Scholarship Pokot Magharibi

Na Benson Aswani,
Wanafunzi 74 wamenufaika na ufadhili wa serikali ya kaunti ya Pokot magharibi kupitia mpango wa ufadhili wa elimu scholarship, karo yao ya shule ikilipwa pamoja na mahitaji mengine ya kimsingi.
Mkurugenzi wa elimu kaunti hiyo Magara Onduso alisema 29 miongoni mwa walionufaika ni wavulana huku wasichana wakiwa 45, wote wakiwa wanaojiunga na gredi ya kumi.
Alisema kando na kuwapa ufadhili wa elimu, wanafunzi hao pia wamepokezwa ushauri nasaha huku akiwahimiza wazazi wa wanafunzi hao pia kuendelea kuwashauri ili wafanye vyema masomoni.
“Tumewafadhili wanafunzi 75 na kati ya hao, tuna wavulana 29 na wasichana 45, na serikali imewekeza zaidi kwenye mpango huu ikiwemo karo na matumizi yao pale shuleni. Tumewashauri wanafunzi hawa vilivyo na pia tunawaomba wazazi kuwashauri pia, ili wasiache jukumu lao kama wazazi,” alisema Onduso.
Aidha, Onduso alisema wanafunzi hao walichukuliwa kutoka kila wadi ili kuhakikisha kuna usawa, wanafunzi waliopata pointi 50 na zaidi wakipewa kipau mbele.
“Tuliwazingatia zaidi wanafunzi ambao walipata pointi 50 na zaidi katika wadi zote ili tuwe na usawa kwenye mpango huo, na tumetembelea maeneo yao ya nyumbani ili kuangazia hali ya uchumi wa familia zao na kama wanastahili ufadhili huu,” alisema.
