Serikali yatakiwa kuanzisha miradi ya maendeleo Bonde la Kerio kudumisha usalama.

Na Benson Aswani,
Seneta wa kaunti ya Pokot magharibi Julius Murgor ametoa wito kwa serikali kuanzisha miradi ya maendeleo maeneo ya mipakani pa kaunti za bonde la kerio hasa baada ya kuanza kushuhudiwa utulivu katika maeneo hayo.


Murgor alisema miradi kama vile ya kilimo kupitia unyunyiziaji maji mashamba itasaidia kuhakikisha wakazi wa maeneo hayo wanapata chakula cha kutosha, na hata kuwasaidia kujikimu kimaisha hali ambayo itapelekea kudumishwa usalama.


Aidha seneta Murgor alisema iwapo miradi ya kilimo itaanzishwa maeneo hayo, itawashughulisha pakubwa hasa vijana ambao ndio hutumika zaidi katika visa vya uvamizi, na kutowapa nafasi ya kufikiria kujihusisha na visa hivyo.


“Baada ya amani kudumishwa, tunapasa sasa kufikiria kile ambacho watu wa hapa watafanya kuendelea kudumisha hali hiyo. Miradi kama vile ya kilimo ambapo wakazi watatumia mbinu ya unyunyiziaji maji mashamab itasaidia pakubwa kuwahusisha na kuhakikisha wana chakula cha kutosha,” alisema seneta Murgor.


Murgor alisema kwamba ni mbinu hiyo ndiyo iliyotumika kuleta amani kati ya jamii za Pokot na Sebei katika taifa jirani la Uganda ambazo sasa zinaishi bila ya mizozo kinyume na awali.


“Jamii za Pokot na Sabiny zimezozana kwa muda, lakini wakati viongozi walielewana kuhakikisha kwamba wakazi wanapata maji na kuendeleza miradi ya kiliomo, hali ilitulia na sasa wanaishi kwa amani,” alisema.