Vijana kutoka jamii za Pokot na Marakwet wadumisha amani kupitia miradi ya kilimo

Na Emmanuel Oyasi,
Hatua ya makundi ya vijana kutoka maeneo ya Cheptulel kaunti ya Pokot magharibi na Kaben kaunti jirani ya Elgeyo marakwet kuja pamoja na kuanzisha miradi ya kilimo imechangia pakubwa katika kukabili swala la utovu wa usalama mipakani pa kaunti hizo mbili.
Kulingana na afisa katika shirika la International alert Doreen Aprich, mmoja wa wafadhili wa vijana hao, hatua ya vijana hao kuja pamoja ni muhimu katika kuleta uwiano baina ya jamii hizo mbili kwani muda wote wanafanya shughuli zao pamoja, akitoa wito kwa washirika wengine kujitokeza na kuwaunga mkono.
“Tunautazama mradi huu kama fursa ya kuafikia amani eneo hilo, kwa sababu unawakutanisha vijana kutoka pande zote mbili katika shughuli za kilimo na biashara na kudumisha uwiano miongoni mwa jamii hizi,” alisema Aprich.
Kwa upande wake afisa wa maswala ya amani na kudhibiti majanga kaunti ya Elgeyo Marakwet Lawrence Mutwol alisema amani ambayo inashuhudiwa maeneo hayo imechangiwa pakubwa na vijana hao ambao mara kwa mara hukutana kuangazia jinsi ya kudumisha amani.
“Nawashukuru vijana hawa kwa sababu wamekuwa katika misitu hii wakitafuta amani, na ni wao ambao wameleta amani hii kwa sababu wamechukua muda kuketi pamoja na kuangazia jinsi ya kuleta usalama eneo hili,” alisema Mutwol.
Kauli yake ilisisitizwa na mkurugenzi wa amani kaunti ya Pokot magharibi kasisi Jackson Alukusia, ambaye alisema hatua hii ni ufanisi mkubwa katika kuleta amani baina ya jamii za kaunti hizo mbili ikizingatiwa historia ya eneo hilo.
“Hatua ya vijana hawa kuja pamoja na kufanya shughuli za kilimo pamoja ni ufanisi mkubwa sana katika juhudi za kuafikia amani eneo hili. Kabla ya hapo eneo hili lilikuwa hatari sana na halingepitika,” alisema Alukusia.
Wakazi wa eneo hilo walipongeza amani ambayo imeendelea kushuhudiwa hali ambayo imewapelekea waliokuwa wamehama maeneo hayo kuanza kurejea baada ya kurejea utulivu.
