Serikali yahimizwa kulainisha usimamizi wa shule za JSS, kuzuia migogoro zaidi

Na Emmanuel Oyasi,
Walimu wa shule za sekondari msingi JSS kaunti ya Pokot Magharibi sasa wanaitaka serikali kupitia wizara ya elimu kulainisha swala la usimamizi wa shule za sekondari msingi, kalenda ya masomo ya mwaka 2026 ikitarajiwa kuanza mwezi januari mwaka ujao ili kuzuia migogoro ambayo ilishuhudiwa mwaka huu baina ya walimu wa JSS na usimamizi wa shule za msingi.
Wakiongozwa na Irene Cheruto, walimu hao wa JSS walisema juhudi zao kuhakikisha viwango bora vya elimu vinatolewa kwa wanafunzi zimekuwa zikihujumiwa na wakuu wa shule hizo ambao ni wakuu wa shule za msingi.
Cheruto alisema uongozi wa shule hizo haujakuwa ukishirikiana na walimu wa JSS kwa kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vya kutumia katika kutoa elimu kwa wanafunzi wa shule hizo kulingana na mahitaji ya mtaala wa elimu CBE.
“Jukumu letu ni kuhakikisha kwamba tunatekeleza mtaala wa elimu darasani, lakini tatizo ni kwamba kuna mahitaji mengi yanayoambatana na mtaala huu ambayo uongozi wa shule za msingi haupo tayari kuhakikisha yanatimizwa,” alisema Cheruto.
Naibu mwenyekiti wa chama cha walimu wa shule za upili na vyuo vya kadri KUPPET tawi la Pokot magharibi Anthony Merisia alitaka walimu hao kupewa uhuru wa kujisimia iwapo serikali inataka kufanikisha malengo ya mtaala wa elimu ya CBE.
“Serikali inapasa kuwapa walimu hawa uhuru wa kujisimamia na kujifanyia maamuzi, ili wahisi kuwa wao ni sehemu ya mfumo mzima wa elimu nchini, iwapo inataka kufanikisha mtaala huu wa CBE,” alisema Merisia.
