Idara ya usalama Pokot Magharibi yaimarisha juhudi za kukabili uhalifu masokoni

Na Emmanuel Oyasi,
Kamanda wa polisi kaunti ya Pokot magharibi Abdulahi Jire amewahakikishia wakazi wa kaunti hiyo kwamba usalama umeimarishwa hasa katika masoko na vituo vya biashara ili kuhakikisha visa vya uhalifu vinakabiliwa.


Katika kikao na wanahabari, Jire alisema visa vya uhalifu huongezeka msimu wa mwezi Desemba ambao huambatana na sherehe nyingi, ila idara ya usalama imeweka mikakati ya kuhakikisha kwamba visa hivi havishuhudiwi tena.


Alisema wameimarisha doria kwenye masoko yote ya kaunti hiyo ili kuwapa wafanyibiashara mazingira bora ya kuendesha shughuli zao za kibiashara bila ya kuwa na hofu ya biashara zao kuvamiwa na wahalifu.


“Tumeimarisha doria kwenye masoko yetu kaunti hii ili tupunguze uhalifu ambao unaanza kuongezeka hasa tunapoelekea msimu wa krimasi ambapo kila mtu anatafuta mbinu za kupata kitu,” alisema Jire.


Wakati uo huo Jire alisema visa vya utovu wa usalama ambavyo vimekuwa vikishuhudiwa mipakani pa kaunti hiyo na kaunti jirani ya Turkana vimepungua katika siku za hivi karibuni kufuatia mikakati ambayo imewekwa na idara ya usalama kukabili hali hiyo.


“Tumeimarisha usalama kwenye mipaka yetu na Turkana ambako kumekuwa kukishuhudiwa utovu wa usalama. Katika siku za hivi karibuni tumeona kwamba visa vya uvamizi vimepungua sana,” alisema.


Jire pia aliwatahadharisha wahudumu wa boda boda kuwa makini hasa baada ya kuripotiwa ongezeko la wizi wa pikipiki ambao unatekelezwa kati ya eneo bungela Kapenguria kaunti ya Pokot magharibi na kaunti Jirani ya Trans nzoia, wanaoutekeleza wakijifanya wateja na kisha kuwavamia wahudumu hao.


Alisema kufikia sasa wamepokea kesi 10 zinazohusu wizi huo, ambapo pikipiki sita tayari zimepatikana huku washukiwa wanne wakinaswa.