Walimu wa JSS waendeleza shinikizo la kutaka kujisimamia

Na Benson Aswani,
Walimu wa shule za sekondari msingi JSS wameendelea kushinikiza shule hizo kuondolewa chini ya usimamizi wa shule za msingi na badala yake kupewa uhuru wa kujisimamia.


Wakiongozwa na Irene Cheruto, walimu hao katika kaunti ya Pokot magharibi walisema hata muundo wa mtaala wa elimu wenyewe unaruhusu shule hizo za JSS kujisimamia kama taasisi huru na kuwa na uongozi wake kando na shule za msingi.


Aidha walimu hao walisema usimamizi baina ya walimu wa shule za msingi na sekondari msingi haujawekwa wazi na serikali kupitia wizara ya elimu, hali ambayo imekuwa ikichangia mivutano baina ya walimu wa JSS na uongozi ambao pia ni wa shule za msingi.


“Muundo wa mtaala huu uko wazi kuhusu jinsi shule za JSS zinapasa kuendeshwa. Sisi kama walimu wa JSS tunapasa kujisimamia kwa sababu migogoro mingi imekuwa ikishuhudiwa baina ya walimu wa JSS na uongozi wa shule kutokana na kutoelewa vyema muundo wa mtaala huo,” alisema Cheruto.

Kauli ya walimu hao ilisisitizwa na naibu mwenyekiti wa chama cha KUPPET tawi la Pokot magharibi Anthony Merisia, ambaye alisema walimu wa JSS wamenyimwa uhuru wa kufanya maamuzi hali ambayo inafanya vigumu kufanikisha malengo ya mtaala wa CBC.


“Walimu wa JSS wamenyimwa jukwaa la kujieleza hali wao ndio wahusika wakuu katika kufanikisha mfumo wa elimu CBC. Ili mfumo huu ufanikiwe, ni lazima walimu hawa wapewe uhuru wa kujitawala na wasiwe chini ya usimamizi wa shule za msingi,” alisema Merisia.