Wakazi Kacheliba walalamikia nafasi chache za usajili wa makurutu wa polisi

Na Emmanuel Oyasi,
Wakazi wa eneo bunge la Kacheliba kaunti ya Pokot magharibi wamelalamikia nafasi chache ambazo eneo hilo lilitengewa katika zoezi la usajili wa makurutu wa polisi ambalo limefanyika jana.
Wakiongozwa na Joseph Sarich, wakazi hao walisema eneo bunge hilo lilitengewa nafasi tatu pekee katika wadi zote jambo ambalo ni kejeli kwa wakazi wa eneo hilo, ikizingatiwa idadi jumla ya makurutu waliotangazwa kusajiliwa kote nchini.
Wakazi hao walisema huenda zoezi hilo lilitekwa nyara na baadhi ya watu ambao waliwatengea watu kutoka maeneo mengine nafasi ambazo zilifaa kukabidhiwa wakazi wa eneo hilo.
“Tulitengewa nafasi tatu pekee katika wadi zote eneo hili. Ni kama sasa wametuambia ni mtu mmoja kutoka kila wadi, jambo ambalo ni kejeli kwetu sisi. Ni kama kuna watu ambao wamechukua nafasi zetu na kuwapa watu wengine,” alisema Sarich.
Alitoa wito kwa serikali kuangazia kwa uzito visa kama hivi anavyosema kwamba huenda vikalemaza sera ya serikali ya kubuni nafasi za ajira kwa wananchi, waathiriwa wakuu wakiwa vijana kutoka jamii masikini.
“Naomba serikali iweze kuchunguza mambo haya ili tuwe na kenya ambayo ni ya kila mtu. Kwa sababu sasa ni kama mtu kutoka jamii masikini hawezi kupata nafasi Kenya hii,” alisema.
Yanajiri haya huku afisa aliyesimamia shughuli hiyo eneo bunge la Kapenguria Francis Nganga akielezea kuridhishwa na idadi ya vijana waliojitokeza katika zoezi hilo.Alisema makurutu 17 walisajiliwa, wavulana 15 huku wasichana wawili wakichukuliwa.
“Vijana wengi walijitokeza katika zoezi hili na liliendelea vizuri bila kuripotiwa changamoto yoyote. Tunawapongeza wale waliofanikiwa kusajiliwa, na wale ambao hawakufanikiwa wasife moyo kwani kuna wakati mwingine,” alisema Ng’ang’a.
