Kaunti ya Turkana yamulikwa kwa kutosalimisha silaha haramu

Na Benson Aswani,
Takriban silaha alfu moja zinazomilikiwa kinyume cha sheria kanda ya kaskazini mwa bonde la ufa zimesalimishwa kufikia sasa kutokana na agizo la serikali, kama njia moja ya kukabili swala la utovu wa usalama kanda hii.


Akizungumza baada ya kuongoza kikao cha usalama eneo la Turkwel kaunti ya Pokot magharibi, kamishina kanda ya bonde la ufa Abdi Hassan hata hivyo alisema kaunti ya Turkana haijatoa ushirikiano unaostahili akiwataka wanaomiliki silaha hizo kuzisalimisha kabla ya kuanza oparesheni ya kuzitwaa kwa nguvu.


“Hivi sasa katika eneo la North Rift kwa jumla tumekaribia alfu moja wale ambao wamesalimisha silaha haramu. Na tunawashukuru sana. Lakini kaunti ya Turkana bado tuna changamoto kwa sababu idadi ambayo inatakikana kutoka kwao, hawajarejesha,” alisema Hassan.


Hassan alionya kwamba hatua za sheria zitachukuliwa dhidi ya mkazi ambaye atapatikana na silaha kinyume cha sheria baada ya kukamilika makataa ambayo yalitolewa na serikali kwa wanaozimiliki kuzisalimisha kwa hiari.


“Tunataka kuwaarifu wale ambao bado wanamiliki silaha haramu kwamba bado wana muda wa kuzisalimisha. Na wale ambao watakaidi amri hii tutawatembelea vilivyo kisheria,” alisema.


Wakati uo huo Hassan alisema matamshi ya kiholela ya viongozi hasa wa kisiasa ndicho kichocheo kikuu cha utovu wa usalama katika kaunti hizo akiwataka kuwa makini na matamshi wanayotoa ili wasiweze kuchochea uhasama baina ya jamii.


“Matamshi ya kiholela ya viongozi ndiyo yanachangia pakubwa uhasama baina ya jamii eneo hili. Na sasa tunawaambia viongozi wetu, wachunge sana matamshi ambayo wanarusha hapa na pale,” alisema.