Poghisio ataka kuimarishwa usalama mipakani, mitihani ya KCSE ikiendelea

Na Benson Aswani,
Aliyekuwa seneta wa kaunti ya Pokot magharibi Samwel Poghisio ameendelea kutoa wito kwa wakazi wa maeneo ya mipakani pa kaunti hiyo na kaunti jirani ya Turkana ambako kumeshuhudiwa kuchipuka tena visa vya utovu wa usalama kuacha kuvamiana na kuzingatia amani.


Poghisio alisema inasikitisha kuona wakazi wasio na hatia wakiuliwa na wahalifu wachache, akiwataka viongozi kutoka pande zote mbili kuketi na kutafuta suluhu ya kudumu kwa ajili ya tatizo hili.

Alisema ni wakati ambapo hatua za dharura zinapasa kuchukuliwa kushughulikia hali hii, hasa ikizingatiwa kwamba kwa sasa watahiniwa wa mitihani ya kitaifa wanaendelea na mitihani yao, na huenda hali ya utovu wa usalama ikaathiri pakubwa shughuli hiyo.


“Visa vya utovu wa usalama mpakani pa kaunti ya Pokot magharibi na Turkana vimezidi sana. Kila siku naona picha za watu wamepigwa risasi. Nataka tuangalie vizuri sana, viongozi wa Pokot magharibi na Turkana, tafadhali tuketi chini tumalize haya maneno,” alisema Poghisio.

Wakati uo huo Poghisio aliwasuta vikali viongozi ambao wanaeneza uchochezi miongoni mwa wananchi hasa kuhusiana na mipaka ya kaunti hizo, akisema jukumu la kubaini mipaka si la wanasiasa bali kuna idara ya serikali ambayo inashughulikia swala hilo na inafaa kuachiwa jukumu lake.


“Haya maneno ya uchochezi ambayo yanatolewa na wanasiasa, mtu anajipiga kifua eti anaweza kusongesha kabila moja kutoka sehemu moja hadi nyingine, kwani wana uwezo gani kufanya hivyo? Mambo kama haya ndiyo yanayochochea uhasama baina ya jamii,” alisema.