Shule ya wavulana ya Kapenguria yapandishwa hadhi na kuwa ya kitaifa

Na Benson Aswani,
Walimu na wazazi wa shule ya upili ya wavulana ya Kapenguria kaunti ya Pokot magharibi wamepongeza hatua ya kupandishwa hadhi shule hiyo kutoka kiwango cha extra county hadi shule ya kitaifa.


Akizungumza baada ya kupandishwa hadhi shule hiyo, mwalimu mkuu Moses Ndeda alisema hatua hii ni muhimu kwani itasaidia shule hiyo kupokea wanafunzi kutoka maeneo mbali mbali ya nchi, hali ambayo itapanua mawazo ya wanafunzi wa shule hiyo kutoka kaunti hii ya Pokot magharibi.

Aidha Bw. Ndeda alisema hatua hiyo itasaidia shule kupata maendeleo yanayohitajika kutokana na hadhi yake.
“Kuna faida nyingi kwa shule kuwa ya kitaifa, kwa kuwa watoto wanatoka sehemu mbali mbali za nchi. Na tukitaka kuwe na maendeleo, ni vizuri kuchanganya watu kutoka sehemu mbali mbali, mawazo mbali mbali na akili mbali mbali,” alisema Bw. Ndeda.


Kauli yake ilisisitizwa na walimu wa shule hiyo wakiongozwa na Zipora Siwatum ambao walisema japo kuna majukumu mengi yanayoambatana na kupandishwa hadhi shule hadi kuwa ya kitaifa, wapo tayari kwa changamoto hiyo kutokana na mazingira bora ambayo yameandaliwa na uongozi wa shule.


“Tunajua kuna mengi ambayo yanatokana na shule kupandishwa hadhi na kuwa ya kitaifa. Na sisi kama walimu tupo tayari kwa changamoto hii na tutafanya juhudi zote ili kudhihirisha kwamba tulistahili kupewa hadhi hii mpya,” alisema Bi. Siwatum.


Ni hatua ambayo ilipongezwa pia na wazazi wa shule hiyo wakiongozwa na Christine Musyoki ambao wameitaja kuchangiwa na juhudi pamoja na uongozi bora wa shule hiyo.