Mpango wa ‘Nyota’ wakosa msisimko uliotarajiwa

Na Benson Aswani,
Idadi ndogo sana ya vijana walijitokeza katika hafla ya uhamasisho kuhusu mpango wa kuwawezesha vijana kiuchumi wa Nyota ambao umehasisiwa na rais William Ruto kwa msaada wa benki ya dunia.
Akizungumza baada ya kuongoza hafla hiyo iliyoandaliwa katika ukumbi wa Mtelo, eneo bunge la Kapenguria kaunti ya Pokot magharibi, katibu katika wizara ya kazi za umma Joel Arumonyang alisema kwamba hali hii imechangiwa na idadi kubwa ya waliotuma maombi ya kunufaika na ufadhili huo kutoafikia masharti yaliyowekwa.
“Kiwango cha chini sana cha vijana walijitokeza kwenye shughuli ya leo ya uhamasisho kuhusu mpango huu wa Nyota. Hii ni kutokana na hali kwamba wengi wa watu waliotuma maombi hawakuafikia masharti. Mpango huu unalenga vijana kati ya miaka 18 na 29, lakini unapata kwamba vijana wengi waliotuma maombi ni wenye zaidi ya umri wa miaka 30,” alisema Arumonyang.
Aidha alitaja changamoto ya miundo mbinu kuwa sababu ya wengi wa vijana kutojitokeza, akisema mikakati inaendelea ya kukabili tatizo hilo, akiwahimiza vijana kuendelea kutuma maombi ili kunufaika na ufadhil huo utakaowawezesha kuinuka kiuchumi.
“Kaunti hii ina changamoto nyingi za miundo mbinu, mitandao na ugumu wa kupata habari kwa wakati. Lakini sasa tumeweka mikakati ya kushughulikia hali hii ili tuweze kupata idadi nzuri ya watakaonufaika na mpango huu,” alisema.
Baadhi ya vijana waliojitekeza kwenye zoezi hilo walipongeza mpango huo waliosema utawawezesha kujikwamua kiuchumi, na kupunguza visa vya wizi wa mifugo katika kaunti hiyo, japo baadhi wakilalamikia masharti yaliyowekwa na serikali hasa kuhusu umri wa wanaopasa kunufaika.