Vyombo vya habari vyatakiwa kuwa msitari wa mbele katika vita dhidi ya ukeketaji

Na Benson Aswani,
Vyombo vya habari vimetakiwa kuchangia katika vita dhidi ya ya tamaduni ya ukeketaji vinavyoendelezwa na serikali kwa ushirikiano na mashirika mbali mbali ya kijamii, kwa kuhakikisha kwamba vinatoa habari za kweli kuhusiana na hali hiyo.


Akizungumza baada ya warsha ya wanahabari iliyoandaliwa katika mkahawa mmoja mjini Makutano kaunti ya Pokot magharibi, mkurugenzi katika idara ya jinsia Emmanuel Oigo alisema kaunti hiyo ni miongoni mwa kaunti ambazo zinaendeleza tamaduni hii kwa viwango vya juu.


“Pokot magharibi ni miongoni mwa kaunti ambazo zimetajwa kuwa na visa vingi vya ukeketaji, na tunaamini kwamba kwa kuhusisha vyombo vya habari tunaenda kukabili tamaduni hii hasa maeneo ya mashinani,” alisema Oigo.


Aidha ni katika warsha hiyo ambapo kuliwekwa mkataba wa ushirikiano kati ya baraza la vyombo vya habari na kituo cha demokrasia na uongozi bora (CEDGG) katika vita vya kukabili ukeketaji kaunti ya Pokot magharibi anavyoeleza Kemunche Masese, afisa katika kituo hicho.


“Lengo kuu la mkatano wa leo ilikuwa kuwekwa mkataba ambao utawezesha kufanya kazi kwa pamoja kati ya wanahabari gatuzi la Pokot magharibi na shirika la CEDGG kukabili hii changamoto ya ukeketaji,” alisema Masese.


Kwa upande wake afisa katika baraza la vyombo vya habari MCK Joseph Mecha alisema wanahabari wana nafasi kubwa katika kuhamasisha jamii dhidi ya tamaduni hiyo.


“Tumejikita leo sana kwenye maswala ya ukeketaji ambapo wanahabari wamehamasishwa jinsi ya kufanya kazi kitaalam, ili kuhakikisha kwamba wanawafahamisha wananchi waweze kuelewa madhara yanayotokana na ukeketaji wa watoto wasichana,” alisema Mecha.