Wakulima watakiwa kukumbatia mbinu za asili za kilimo

Na Emmanuel Oyasi,
Wakulima katika kaunti ya Pokot magharibi wameshauriwa kukumbatia mbinu za kiasili katika kuendeleza shughuli zao za kilimo kama njia moja ya kuimarisha mazao na kuhifadhi mazingira.


Wito huu umetolewa na shirika la Ripple effect ambalo limekuwa likiendeleza mafunzo kwa wakulima maeneo mbali mbali ya kaunti hiyo kuhusu haja ya kutumia mbolea ya kiasili, pamoja na dawa za kunyunyizia mimea, zisizo za kemikali.


Afisa wa shirika hilo Kennedy Molo alisema mbinu hii ya ukulima inasaidia pakubwa kupunguza kemikali kwenye mchanga pamoja na kwenye mimea na hivyo kuwaepushia wakazi matatizo ya kiafya ambayo yanatokana na kemikali nyingi kwenye chakula.


“Jambo ambalo huwa la kwanza katika kila eneo tunaenda ni kuunda mbolea ya asili. Hii ni mbolea ambayo itasaidia kupunguza kemikali kwenye mchanga, ambayo inatokana na mbolea ambayo tunanunua madukani,” alisema Molo.


Kauli yake ilisisitizwa na mkurugenzi wa kilimo kaunti hiyo Philip Ting’aa ambaye aidha aliwahimiza wakazi wa kaunti hiyo kukumbatia kilimo cha mimea tofauti na kutoegemea kilimo cha mahindi pekee ili kuwe na usalama wa chakula.


“Mara nyingi watu hufikiria kwamba kuwa na mahindi labda tuna usalama wa chakula, ila tunafaa kufahamu kwamba lazima tupande aina nyingi ya vyakula ndipo tuseme tumeweza kuwa na usalama wa chakula katika kaunti yetu,” alisema Ting’aa.


Baadhi ya wakulima katika kaunti hiyo wakiongozwa na Philip Kopirpir walipongeza mafunzo ambayo wamepokea kutoka kwa shirika hilo waliyosema yamewawezesha kuimarisha shughuli zao za kilimo.