Vita dhidi ya ujangili vyashika kasi Pokot Magharibi

Na Benson Aswani,
Kamishina wa kaunti ya Pokot magharibi Khalif Abdulahi ameendeleza wito kwa wakazi wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kuzirejesha kabla ya kukamilika makataa ya mwezi mmoja yaliyotolewa na waziri wa usalama na maswala ya ndani ya nchi Kipchumba Murkomen.


Akizungumza baada ya kupokea jumla ya bunduki 3, 2 aina ya AK 47 na moja aina ya FN pamoja na risasi 12 zilizosalimishwa na wakazi kutoka maeneo ya Chepkokough na Nyang’aita, Khalif aliwahakikishia usalama wale wote ambao watasalimisha silaha hizo, akisema watahusishwa katika mipango ya serikali kuimarisha hali yao ya uchumi.


“Tunaenda kuhakikisha kwamba wale wanaosalimisha silaha zao watanufaika na miradi ya serikali, ikiwemo kupokea mafunzo ya kiufundi na kujumuishwa kwenye mradi wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu ili waweze kujikimu kimaisha baada ya kuasi uhalifu,” alisema Khalif


Aidha Khalif alisema oparesheni ya kutwaa silaha hizo kwa nguvu itaanzishwa baada ya kukamilika makataa yaliyotolewa na waziri Murkomen, akionya kwamba wale ambao watapatikana wakimiliki silaha hizo watakabiliwa vikali kisheria.


“Baada ya kukamilika makataa yaliyotolewa na waziri wa usalama, tutaanza oparesheni ya kutwaa silaha hizo kwa nguvu. Na wale ambao watapatikana nazo watachukuliwa hatua za kisheria,” alisema.


Naibu kamishina eneo la pokot ya kati Jeremia Tumo alipongeza mkakati wa usalama ambao umewekwa wa kuwatambua baadhi ya wamiliki wa silaha haramu hali ambayo imesaidia kupatikana bunduki hizo.


“Baada ya kikao na waziri wa usalama tuliweka mkakati wa kuwatambua wale ambao tunashuku wanamiliki silaha hizi, na hatua hii imetusaidia kupata silaha hizi,” alisema Tumo.


Kwa upande wake mkurugenzi wa amani kaunti ya Pokot magharibi kasisi Jackson Alukusia alisema kuwepo nia ya kusalimisha silaha ambazo zinamilikiwa na baadhi ya wakazi kinyume cha sheria ni ufanisi mkubwa kwa amani ya eneo zima la bonde la Kerio.


“Hatua hii ni ufanisi mkubwa kwa usalama wa eneo hili na eneo zima la bonde la Kerio. Kwa hivyo tunawapongeza wale ambao wamesalimisha silaha zao,” alisema Alukusia.