Wahalifu warejelea shughuli zao Songok

Na Benson Aswani,
Chifu wa eneo la Songok mpakani pa kaunti ya Pokot magharibi na kaunti jirani ya Turkana Joseph Korkimul amesikitikia kuchipuka tena visa vya utovu wa usalama mpakani pa kaunti hizo mbili.

Akizungumza na kituo hiki Korkimul alisema visa hivyo ambavyo vilianza na wizi wa mifugo sasa vimegeuka kuwa mauaji yanayolenga wakazi wa maeneo hayo, akitoa wito kwa serikali kupitia idara ya usalama kuingilia kati na kukabili wahalifu wanaoendeleza visa hivyo.


Aidha Korkimul alidai kuwa visa hivyo vimechochewa na viongozi wa kisiasa anaodai wanashirikiana na wahalifu kuwalenga watu fulani wenye ushawishi miongoni mwa jamii hasa wa upande wa pokot magharibi.


“Hali ya usalama imeendelea kudorora eneo hili. Hali hii ilianza na wizi wa mifugo na sasa imegeuka na kuanza kuwalenga wakazi. Kuna baadhi ya wanasia ambao wanawatumia wahalifu kuwalenga wakazi ambao wana ushawishi katika jamii upande wa Pokot,” alisema Korkimul.


Korkimul alidai visa hivi vya utovu wa usalama vimechochewa na hatua ya maafisa wa usalama kutepetea katika majukumu yao, punde baada ya hali ya utulivu kurejea maeneo hayo, swala ambalo liliwapa mwanya wahalifu kurejelea visa vya wizi wa mifugo.


“Msako ambao ulitekelezwa eneo hili na maafisa wa polisi kwa ushirikiano na wale wa KDF ulisaidia sana kukabili visa hivi. Lakini walifika mahali wakatulia, na ndio maana wahalifu wakarejelea wizi wa mifugo,” alisema.