Moroto aahidi kuhakikisha umeme unafika kila sehemu eneo bunge la Kapenguria

Na Emmanuel Oyasi,
Mbunge wa Kapenguria kaunti ya Pokot magharibi Samwel Moroto amewahakikishia wakazi wa eneo bunge lake kwamba atahakikisha umeme unafika maeneo ambako kuna changamoto hiyo.
Moroto alisema atatumia kipindi cha majuma mawili ambapo bunge litaenda mapumzikoni, kinachotarajiwa kuanza tarehe 15 mwezi huu kutembelea kila eneo la eneo bunge lake kuhakikisha kila mkazi anafikiwa na umeme.
Moroto aliwataka wakazi wa maeneo mbali mbali ya eneo bunge lake kushirikiana na maafisa ambao watakuwa wakitekeleza shughuli ya kuunganisha umeme, ili kuhakikisha kwamba huduma hiyo inawafikia bila ya vizingiti vyovyote.
“Bunge linaenda mapumzikoni kuanzia tarehe 15. Katika kipidi hicho cha wiki mbili, nitazunguka huku kote na watu wa kampuni ya Kenya power kuhakikisha kwamba kila mtu anapata umeme. Naomba tu watakapokuja tushirikiane nao kikamilifu,” alisema Moroto.
Wakati uo huo Moroto alitumia fursa hiyo kuwahakikishia wakazi kwamba shughuli ya kuwaajiri walimu pamoja na maafisa wa polisi itaanza mwezi Octoba, akisema shughuli hiyo ilichelewa baada ya mswada wa fedha kutupiliwa mbali mwaka jana kufuatia maandamano ya vijana wa kizazi cha Gen-Z.
“Shughuli ya uajiri wa watu, polisi na walimu itaanza mwezi Octoba kwa sababu bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 itaanza kuzunguka sasa mwezi huu, baada ya mswada wa fedha wa kipindi cha fedha ambacho kilikamilika kutupiliwa mbali kufuatia maandamano ya Gen-Z,” alisema.