Mikakati ya kuimarisha usalama Pokot Kaskazini yaendelea

Na Benson Aswani,
Idara ya usalama kaunti ya Pokot magharibi inaendelea kuweka mikakati ya kukabili visa vya utovu wa usalama katika baadhi ya maeneo ya eneo la Pokot kaskazini ambako kumeripotiwa visa kadhaa vya wizi wa mifugo.
Akizungumza na wanahabari kamanda wa polisi kaunti hiyo Mohammed Jire alisema kwamba wameandaa kikao na maafisa wa akiba NPR maeneo ya Ramos, Ombolion na Morita ambapo alisema wameongeza silaha ambazo zitapiga jeki doria za maafisa hao.
“Nia ya ziara yangu ilikuwa kukutana na maafisa wa NPR na kukagua hali ya usalama eneo hilo. Kuna takriban visa 23 vya wizi wa mifugo ambavyo vimeripotiwa. Tumeangazia jinsi ya kuimarisha usalama ambapo pia tumeongeza silaha ambazo zitasaidia katika doria zao,” alisema Jire.
Wakati uo huo Jire alitoa wito kwa wakazi wa eneo hilo kushirikiana na maafisa wa usalama katika kuhakikisha kwamba usalama unadumishwa kwa kutoa taarifa muhimu kwa maafisa hao kuhusiana na watu ambao wanaendeleza visa vya wizi wa mifugo.
“Nawasihi tu wananchi wa maeneo haya washirikiane na maafisa hawa kwa kutoa taarifa muhimu zitakazosaidia kuwakabili wanaoendeleza wizi wa mifugo na kupelekea utovu wa usalama,” alisema.
Aidha Jire alisema ombi la wakazi la kutaka kambi ya maafisa wa NPR kujengwa eneo hilo limepokelewa na kwamba amekutana na gavana wa kaunti hiyo Simon Kachapin ambapo amekubali kujenga kambi hiyo ili kuimarisha usalama wa eneo hilo.
“Nimekutana na gavana katika afisi yake na tukazungumza kuhusu kujengwa kambi ya maafisa hawa maeneo athirika, na akaahidi kutusaidia kuhakikisha kwamba kambi hiyo inakuwepo,” aliongeza.